Kinara wa upinzani wa Sudan Kusini 'azuiwa' kushiriki mkutano wa Vatican
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52750-kinara_wa_upinzani_wa_sudan_kusini_'azuiwa'_kushiriki_mkutano_wa_vatican
Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar ameripotiwa kuzuiwa kwenda Vatican, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani nchini Italia kushiriki mkutano wa amani kati yake na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 10, 2019 07:53 UTC
  • Kinara wa upinzani wa Sudan Kusini 'azuiwa' kushiriki mkutano wa Vatican

Kiongozi wa upinzani wa Sudan Kusini, Riek Machar ameripotiwa kuzuiwa kwenda Vatican, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani nchini Italia kushiriki mkutano wa amani kati yake na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Brazille Musumba, msemaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema ingawaje jumuiya hiyo inaunga mkono jitihada zozote za kuleta amani ya kudumu nchini Sudan Kusini, lakini ombi la Machar la kuruhusiwa kwenda kushiriki mkutano wa Vatican halijaidhinishwa kufikia sasa.

Hata hivyo msemaji wa Kiir, Ateny Wek Ateny amesema rais huyo wa Sudan Kusini aliekea Vatican jana Jumanne kushiriki mkutano huo, na kwamba Machar pia ameondoka Khartoum mji mkuu wa Sudan, ambako amekuwa akiishi, kwenda kushiriki kikao hicho cha Vatican.

Mahasimu hao wawili wa kisiasa wa Sudan Kusini walitazamiwa kukutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mwezi Septemba mwaka jana, katika mkutano huo wa Vatican, uliokuwa ufanyike jana Jumanne na leo.

Hii ni katika hali ambayo, Riek Machar anatazamiwa kurejea nchini Sudan Kusini mwezi ujao, chini ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwezi Septemba mwaka jana huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Rais Kiir (kulia) na Riek Machar

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini mwezi uliopita, ambapo aliahidi kwamba karibuni hivi ataitembelea nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kwa lengo la kusukuma mbele mchakato wa amani.

Nchi ya Sudan Kusini iliyojitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani, Disemba mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni wamelazimika kuwa wakimbizi.