Interpol yaokoa makumi ya watoto kutoka katika masoko ya utumwa Afrika Magharibi
Polisi ya Kimataifa (Interpol) imefanikiwa kuwanusuru makumi ya watu aghalabu yao wakiwa ni watoto, waliokuwa katika masoko ya utumwa katika nchi mbili za Afrika Magharibi.
Paul Stanfield, Mkurugenzi wa Interpol katika masuala ya jinai ibuka na za kuratibiwa amesema kuwa, watu 216, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo wameokolewa katika operesheni ya pamoja iliyofanywa na polisi za Benin na Nigeria.
Amesema operesheni hiyo kwa jina Epervier II iliyohusisha askari polisi 100 kutoka nchi mbili hizo za magharibi mwa Afrika, ilifanyika mapema mwezi huu wa Aprili.
Stanfield ameuambia Wakfu wa Thomson Reuters kwamba, miongoni mwa waliokolewa katika operesheni hiyo ni watoto 157. Amesema watoto hao walikuwa wanafanyishwa kazi za sulubu na baadhi yao wakitumiwa katika mambo ya ufuska kama ukahaba.
Amesema watoto waliookolewa katika opersheni hiyo wenye umri wa miaka 11 hadi 16 wanatokea katika nchi za Benin, Burkina Faso, Niger, Nigeria na Togo.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani (ILO) lilisema utumwa bado ni tatizo kubwa linalowaathiri zaidi ya watu milioni 40 duniani kote, huku watoto wakiwa ni robo ya idadi hiyo.