Polisi wa Nigeria watuhumiwa kuwabaka washukiwa wa ukahaba
(last modified Tue, 07 May 2019 07:36:13 GMT )
May 07, 2019 07:36 UTC
  • Polisi wa Nigeria watuhumiwa kuwabaka washukiwa wa ukahaba

Jeshi la Polisi la Nigeria linachunguza madai kuwa baadhi ya maafisa wake waliwabaka mamia ya wanawake waliowakamata kwa tuhuma za kujihusisha na ukahaba.

Usman Umar, Naibu Kamishna wa Polisi mjini Abuja amesema uchunguzi umeanzishwa kubaini madai hayo, na kwamba afisa yeyote wa polisi atakayepatikana na hatia ya kujihusisha na unyanyasaji huo wa kijinsia atakabiliwa na mkono wa sheria.

Polisi ya Nigeria imelazimika kuchunguza madai hayo baada ya makundi ya kiraia na watetezi wa haki za binadamu nchini humo kufanya maandamano wakitaka wahusika wa jinai hiyo wapandishwe kizimbani.

Aidha watetezi za haki za binadamu nchini humo wamekuwa wakifanya kampeni katika mitandao ya kijamii ya kushinikiza kuchukuliwa hatua za kisheria maafisa wanaotuhumiwa kuhusika na ufuska huo.

Maafisa usalama nchini Nigeria

Mwishoni mwa mwezi uliopita, polisi ya Nigeria ilifanya msako nyakati za usiku na kuwatia mbaroni wanawake zaidi ya 200, ikiwatuhumu kuwa ni mahakaba. Mwanachuo mmoja mwenye umri wa miaka 27 ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema maafisa hao wa polisi waliwafanyia kila aina ya ufuska walipowakamata.

Marcelle Umar, mwanachama wa asasi za kupambana na ubakaji ya 'Coalition to End Rape' amesema, "ni jambo la kusikitisha namna maafisa usalama wanavyowalenga tu wanawake wakiwatuhumu kujihusisha na ukahaba, huku wakiwaacha wanaume wanaojihusisha na uozo huo wa kijamii."