Watu 3 wauawa katika shambulio la Daesh (ISIS) kusini mwa Libya
Kwa mara nyingine tena kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetumia mwanya uliosababishwa na mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vile vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar nchini Libya, kutekeleza shambulio kusini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watu wanaosadikiwa kuwa wanachama wa Daesh wameshambulia mji wa Ghadwa ulioko kusini mwa nchi na kuua watu watatu, kabla ya kutoroka na kurejea katika maficho yao katika mji huo wa jangwani.
Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, hii ni hujuma ya pili kutekelezwa na magaidi hao wakufurishaji katika siku za hivi karibuni.
Mwezi uliopita, kundi hilo lilitangaza kuhusika na mauaji ya watu watatu katika shambulio jingine lililolenga mji wa Fuqaha ulioko kusini mwa Tripoli, unaodhibitiwa na vikosi vitiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar.

Tarehe 4 Aprili mwaka huu, Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri kwa wapiganaji wake ya kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 430 wameshauawa na zaidi ya 2000 wengine wamejeruhiwa tangu yalipoanza mashambulizi hayo.
Watu 55 elfu wengine wanakadiriwa kukimbia makazi yao kutokana na vita hivyo.