May 14, 2019 11:52 UTC
  • Kuendelea mapigano nchini Libya; tishio kwa usalama wa kimataifa

Sambamba na kuendelea mapigano nchini Libya na kupanuka wigo wake, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya wametoa taarifa iliyoyataja mashambulio ya jeshi la taifa la Libya dhidi ya mji mkuu Tripoli na viunga vyake kwamba ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba, mapigano hayo ni tishio kwa uthabiti wa Libya na hivyo imezitaka pande husika kuhitimisha vita na mapigano katika mji mkuu Tripoli. Duru mpya ya mapigano nchini Libya ilianza tarehe 4 ya mwezi uliopita wa Aprili baada ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar kuanzisha mashambulio vikisonga mbele kuelekea katika mji mkuu Tripoli.

Zaidi ya watu 454 wameuawa na wengine 2154 kujeruhiwa, tangu kuanza mapigano hayo mjini Tripoli na viunga vyake. Farhan Haq, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadhrisha kwamba: Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya nchini Libya kufuatia mapigano katika mji mkuu Tripoli pamoja na viunga vyake.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, hali ya mambo nchini Libya inazidi kuwa mbaya. Kuanza vita na kuendelea kwake kumevuruga kabisa mahesabu ya kisiasa pamoja na juhudi za kieneo na kimataifa zilizokuwa na lengo la kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo. 

Jenerali Khalifa Haftar

Kabla ya hapo ilikuwa imepangwa kufanyika mikutano kwa ajili ya kuandaa uwanja na mazingira  ya kufanyika uchaguzi na hivyo kuingia madarakani serikali mpya kupitia njia ya kidemokrasia. Hata hivyo mashambulio ya vikosi vitiifu kwa jenerali Khalifa Haftar yanayofanyika kwa himaya na uungaji mkono wa utawala wa Saudi Arabia na Imarati ambayo lengo lake ni kuudhibiti mji mkuu Tripoli na hivyo kuandaa uwanja wa kuitia mkononi nchi hiyo, yameufanya mgogoro wa nchi hiyo kuingia katika hatua mpya.

Filihali, ni zaidi ya mwezi mmoja sasa ambapo mapigano hayo yameshadidi na kushika kasi. Kusimama kidete Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya kinyume na matarajio ya jenerali Haftar kumevifanya vita na mapigano hayo yaendelee kushuhudiwa. Hii ni katika hali ambayo, kuongezeka idadi ya wakimbizi, uwezekano wa kurejea kundi la kigaidi la Daesh na kushadidi harakati za wanachama wa kundi hilo sambamba na kuongezeka uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ni mambo ambayo yameifanya jamii ya kimataifa izidi kuingiwa na wasiwasi.

Fayez al-Sarraj, Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya ameashiria uungaji mkono wa Misri, Imarati na Saudi Arabia kwa jenerali Khalifa Haftari na kusema kuwa, tunazitaka nchi hizi ambazo zingali zinaviunga mkono vikosi vya jenerali Haftar zitazame upya misimamo yao na kuwapa nafasi wananchi wa Libya.

Fayez al-Sarraj, Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya

Sambamba na kuendelea mapigano nchini Libya, hivi sasa kumeongezeka mashauriano ya kimataifa  kuhusiana na Libya, kiasi kwamba, Jumatatu ya jana kadhia ya Libya ilikuwa miongoni mwa ajenda kuu za mkutano wa Brussels na kulifanyika mazungumzo baina ya viongozi wa nchi hiyo na maafisa wa Umoja wa Ulaya.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya sanjari na kuashiria kwamba, operesheni ya kijeshi nchini Libya inavuruga mazingira ya kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo, ametoa wito wa kuweko usitishaji vita wa haraka na kuepuka aina yoyote ile ya operesheni ya kijeshi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Msimamo wa viongozi wa Ulaya unatolewa katikka hali ambayo, baadhi ya nchi za bara hilo kama Ufaransa ilikuwa muungaji mkono wa jenerali Khalifa Haftar tangu kuanza vita hivyo, lakini hivi sasa kutokana na kuibuka wimbi jipya la wakimbizi na wahajiri kuelekea Ulaya na kuweko uwezekano wa kuongezeka usalama kutokana na harakati za kundi la kigaidi katika eneo, viongozi wa Ulaya  kupitia msimamo wao huu wa kindumakuuwili wanafanya juhudi za kuweko mazungumzo ya kusitishwa vita nchini Libya.

Mapigano nchini Libya

Kutokea maafa ya kibinadamu nchini Libya kwa sasa ndio daghadagha na wasiwasi mkubwa wa maafisa wa jumuiya za kimataifa na ni kwa sababu hii ndio maana wanataka kuweko usitishaji vita nchini humo.

Inaonekana kuwa, mgogoro wa Libya unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuweko ushirikiano wa vikosi vya ndani na mazungumzo ya pande mbili zinazopigana ambayo yatasimamiwa na Umoja wa Mataifa. Hapana shaka kuwa, hatua hiyo itaandaa uwanja wa kufikiwa mwafaka na wakati huo huo kukata mikono ya uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Libya na hatimaye kuiokoa nchi hiyo na hali ya kugawanyika pakubwa.

Tags