Madaktari wasio na mipaka (MSF) wakabiliana na ukosefu wa usalama huko Niger
Wafanyakazi wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) nchini Niger wamelazimika kuondoka kusini mashariki mwa nchi hiyo kutokana na ukosefu wa usalama.
Abdulaziz Mohammed Mkuu wa timu ya Jumuiya hiyo ya Madaktari Wasio na Mipaka huko Niger ameeleza kuwa wafanyakazi wa jumuiya hiyo wamelazimika kuondoka katika mji wa Maine Soroa kusini mashariki mwa nchi kwa sababu za kiusalama. Amesema, MSF imelazimika kusitisha huduma zake za kitiba na kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo miezi mitatu baada ya watu wenye silaha kushambulia ofisi yao katika mji wa Maine Soroa katika mkoa wa Diffa kusini mashariki mwa Niger.
Amesema timu yao ya madaktari imefanya kazi katika mji wa Maine Soroa tangu mwaka 2017. Mji wa Maine Soroa huko Niger unapakana na Nigeria na umekuwa ukilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya wanamgambo wa Boko Haram. Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) inatoa huduma za kitiba na kibinadamu katika maeneo sita huko Niger kwa kusaidiwa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo. Lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto na akinamama pamoja na kutoa huduma kwa wakimbizi.
