Umwagaji damu waendelea Burundi, watu wengine 4 waua
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5539-umwagaji_damu_waendelea_burundi_watu_wengine_4_waua
Watu wanne wameuawa katika matukio mawili tofauti katika kile kinachoonekana ni mauaji ya kulipiza kisasi kati ya maafisa wa serikali na waasi nchini Burundi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2016 10:53 UTC
  • Umwagaji damu waendelea Burundi, watu wengine 4 waua

Watu wanne wameuawa katika matukio mawili tofauti katika kile kinachoonekana ni mauaji ya kulipiza kisasi kati ya maafisa wa serikali na waasi nchini Burundi.

Moise Nkurunziza, Naibu Msemaji wa Polisi wa Burundi amesema kuwa, katika tukio la kwanza, kundi la wabeba silaha limemuua Kanali Emmanuel Buzubona, afisa mwandamizi wa jeshi la nchi hiyo kwa kumshambulia kwa guruneti akiwa kwenye pikipiki akielekea nyumbani kwake jijini Bujumbura. Aidha mwendesha pikipiki aliyekuwa amembeba mwanajeshi huyo aliuawa katika tukio hilo la jana Jumatano.

Katika tukio jingine, waasi wanaoipinga serikali ya Rais Pierre Nkurunziza waliuawa hapo jana katika tukio la ufyatulianaji risasi kati yao na maafisa usalama katika kijiji cha Kivumu, wilaya ya Mugamba Kusini, yapata kilomita 60 kusini mashariki mwa mji mkuu Bujumbura. Watu wanne wa chama tawala cha CNDD-FDD waliuawa katika kijiji hicho wiki iliyopita.

Wizara ya Usalama wa Umma nchini Burundi imetangaza habari ya kuendelea machafuko katika maeneo tofauti ya nchi, ambapo watu zaidi ya 50 wameuawa tokea mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 pekee.

Mamia ya watu wameuawa na maelfu ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi hiyo, tangu Burundi itumbukie katika mchafukoge mwezi Aprili mwaka jana, kufuatia hatua ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea tena urais katika uchaguzi uliopita nchini humo.