Burundi yawatimua raia wa nchi zilizosimamisha ushirikiano na Bujumbura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5587-burundi_yawatimua_raia_wa_nchi_zilizosimamisha_ushirikiano_na_bujumbura
Burundi imewataka raia wa nchi za kigeni zilizosimamisha ushirikiano na serikali ya Bujumbura, kuondoka nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 22, 2016 15:15 UTC
  • Burundi yawatimua raia wa nchi zilizosimamisha ushirikiano na Bujumbura

Burundi imewataka raia wa nchi za kigeni zilizosimamisha ushirikiano na serikali ya Bujumbura, kuondoka nchini humo.

Makamu wa Rais wa Burundi, Gaston Sindimwo amewataka raia wa nchi zilizosimamisha ushirikiano na nchi hiyo kuondoka Burundi au kuomba viza ya utalii. Sindimwo amesema baadhi ya nchi zimeiwekea vikwazo Burundi ikiwa ni pamoja na kusimamisha ushirikiano lakini raia wao wangali wanaishi nchini humo licha ya ofisi za nchi hizo kufungwa.

Mwezi uliopita Umoja wa Ulaya ulisimamisha misaada yake kwa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu ili kumlazimisha kiongozi huyo aketi kwenye meza ya mazungumzo na wapinzani wake. Awali pia Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa (Francophone) ilisimamisha ushirikiano na uhusiano wake na Burundi. Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo ilisema kuwa: Licha ya ahadi zilizotolewa na serikali ya Burundi lakini hakuna hatua ya maana iliyochukuliwa kwa ajili ya kutayarisha mazingira ya kufanyika mazungumzo na kambi ya upinzani; kwa msingi huo na kwa kutilia maanani hali mbaya na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Burundi, jumuiya ya Francophone imeamua kusimamisha ushirikiano na uhusiano wake na serikali ya Burumbura ili kuishinikiza kufanya mazungumzo na wapinzani.

Wakati huo huo ghasia na machafuko yanaendelea kuripoti nchini Burundi. Siku chache zilizopia watu wasiojulikana walishambulia mkahawa mmoja karibu na kituo cha polisi mjini Bujumbura na kuua watu kadhaa.

Machafuko ya Burundi yalianza mwezi Aprili mwaka jana kutokana na upinzani wa umma dhidi ya hatua ya kiongozi wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza ya kuamua kuwania kwa mara ya tatu kiti cha Rais wa Jamhuri. Hadi sasa makumi ya watu wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika ghasia na machafuko hayo. Wapinzani wengi pia wametiwa nguvuni ambapo ripoti zinasema wanapewa mateso makali.

Wiki iliyopita Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alitahadharisha kuhusiana na kuongezeka utumiaji mabavu na vitendo vya kuteswa wapinzani katika nchi ya Burundi. Zeid Ra'ad al-Hussein alisema katika ripoti yake kwamba tangu mwezi Januari mwaka huu kumeripotiwa kesi 345 za kuteswa na kunyanyaswa raia nchini Burundi.

Umoja wa Mataifa na jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu pia zimetahadharisha kuhusu kutiwa nguvuni raia, kuteswa, kupotezwa na kuuawa bila ya kufikishwa mahakamani nchini Burundi.