Wamisri waanzisha kampeni ya kupinga kutolewa visiwa viwili kwa Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5632-wamisri_waanzisha_kampeni_ya_kupinga_kutolewa_visiwa_viwili_kwa_saudia
Wanasiasa na wanaharakati wa Misri wameanzisha kampeni ya kupinga hatua ya Rais wa nchi hiyo, Adul Fattah al Sisi ya kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 23, 2016 01:48 UTC
  • Wamisri waanzisha kampeni ya kupinga kutolewa visiwa viwili kwa Saudia

Wanasiasa na wanaharakati wa Misri wameanzisha kampeni ya kupinga hatua ya Rais wa nchi hiyo, Adul Fattah al Sisi ya kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir.

Vyama mbalimbali vya Misri kikiwemo chama cha Katiba kinachoongozwa na mkurugenzi wa zamani wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Muhammad el Baradei vimetoa taarifa vikitangaza kuwa, vimeanzisha kampeni ya wananchi ya kulinda ardhi ambayo imepewa jina la "Misri Haiuzwi".

Taarifa hiyo imesema kuwa, kampeni hiyo imeanzishwa kupinga hatua ya al Sisi ya kuipatia Saudi Arabia visiwa vya Tiran na Sanafir, na vyama vilivyotia saini taarifa hiyo vimetangaza upinzani wao dhidi ya makubaliano ya kuchora mipaka kati ya Cairo na Riyadh.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, kampeni hiyo itawashinikiza wabunge wa Misri wasikubali makubaliano hyo.

Vyama na makundi mbalimbali ya kisiasa ya Misri yamemkosoa vikali kiongozi wa sasa wa nchi hiyo kwa kuonesha udhaifu mbele ya mfalme Salman wa Saudia na kusema hatua ya kuipatia Riyadh visiwa hivyo imefanyika kinyume cha sheria.