UN: Rwanda imewapokea wakimbizi 189 kutoka Libya
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, Rwanda imewapokea wakimbizi 189 kutoka Libya kufikia sasa.
UNHCR imetuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter unaosema kuwa, "Wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi wapatao 189 wametua salama salmin katika kituo cha Gashora huku suluhulu ikiendelea kutafutwa."
Kundi la kwanza la wakimbizi 66 wakiwemo watoto, akina mama na watu wanaohitaji msaada wa haraka, ambao wamekuwa wakizuiwa nchini Libya, liliwasili Kigali mji mkuu wa Rwanda, na kupelekwa katika kambi hiyo ya Gashora iliyoandaliwa kwa ajili yao, mashariki mwa nchi hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba.
Mapema mwezi jana, Rwanda ilitia saini mkataba na Umoja wa Afrika na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), kwa nchi hiyo kuwakarabisha wakimbizi kutoka mataifa ya Afrika waliokwama nchini Libya wakiwa njini kwenda barani Ulaya.
Serikali ya Rwanda imesema iko tayari kuwapa hifadhi wakimbizi 30,000 kati ya 42,000 wanaozuiwa nchini Libya lakini itawakaribisha kwa utaratibu maalumu na kwa hatua kadhaa, ili kuzuia nchi hiyo yenye watu Milioni 12 isiwe na mzigo.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi nchini Libya, haswa wakimbizi na wahajiri karibu elfu sita wanaozuiliwa katika vituo mbalimbali nchini Libya.