Magaidi 19 wauawa katika oparesheni ya jeshi la Mali
(last modified Mon, 18 Nov 2019 07:26:48 GMT )
Nov 18, 2019 07:26 UTC
  • Magaidi 19 wauawa katika oparesheni ya jeshi la Mali

Jeshi la Mali ilimetangaza kuwa limewauwa magaidi 19 katika oparesheni zake mbili katikati mwa nchi hiyo.

Jeshi la Mali limetoa taarifa na kutangaza kuwa oparesheni hizo zilianza kutekelezwa Ijumaa iliyopita katikati mwa nchi hiyo na kwamba magaidi waliolengwa kwenye mashambulizi hayo walikuwa wakituhumiwa kutekeleza shambulizi Jumatano iliyopita dhidi ya jamii ya Waislamu wa kabila la Fulani ambapo waliwaua wanavijiji wawili. 

Mwezi uliopita pia magaidi waliushambulia msafara wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Mali na kupelekea kuuawa wanajeshi kadhaa wa kikosi hicho cha kulinda amani baada ya kulipuka bomu lililokuwa limetegwa na magaidi hao kando ya barabara.  

Kikosi cha kulinda amani cha UN nchini Mali

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba pia wanajeshi 25 wa Mali waliuawa katika shambulio la magaidi wenye silaha. Kundi lenye misimamo ya kufurutu ada lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida kwa jina la AKIM lilitangaza kuhusika na shambulio hilo. 

Eneo la kaskazini mwa Mali limekumbwa na hali ya mchafukoge tangu mwaka 2012; na kumejitokeza makundi mbalimbali ya wanamgambo wenye silaha na yale yenye kufurutu ada kufuatia kujiri mapinduzi.