Nov 21, 2019 07:35 UTC
  • Mahabusu katika jela za Misri
    Mahabusu katika jela za Misri

Ripoti iliyotayarishwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kwa kushirikiana na Kituo cha Shihab na tasisi ya Uadilifu kwa Ajili ya Haki za Binadamu imesema kuwa, idadi ya jela nchini Misri imefikia 68 na kwamba jela 26 kati yazo zimejengwa katika kipindi cha utawala wa Rais wa sasa wa nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al Sisi.

Ripoti hiyo imesema kuwa idadi ya watu waliopotezwa na kutoweka imefikia 5500 na kwamba idadi ya vituo vya kushikilia watuhumiwa haijulikani nchini Misri.

Mwanasheria Toby Cadman wa taasisi ya Guernica 37 ya kutetea haki za binadamu yenye makao yake London nchini Uingereza amesema kuwa, takwimu zinazohusiana na hali mbaya ya haki za binadamu nchini Misri zinatisha hususan baada ya Abdel Fattah al Sisi kushika madaraka ya kuongoza nchi hiyo. Cadman ameashiria ukandamizaji wa haki za kimsingi za kiraia nchini Misri na ongezeko la kutiwa mbaroni watuhumiwa, kuteswa katika jela na kupotezwa wengine na kusisitiza kuwa, ukiukwaji wa haki za binadamu umeongeza sana nchini Misri tangu Abdel Fattah al Sisi aliposhika madaraka ya nchi. Amesema kuwa kiongozi huyo anaongoza nchi kwa ukatili kubwa kupita hata ule uliosuhudiwa katika utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.

Mohammad Morsi

Toby Cadman amesema kuwa rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia, Mohammad Morsi pia aliuawa na utawala wa sasa wa nchi hiyo kupitia njia ya kumnyima dawa na huduma za tiba akiwa jela. Cadman ameutaka Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi huru kuhusu kifo cha Morsi.

Cadman amesisitiza kuwa Abdel Fattah al Sisi anaendeleza ukatili na mauaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake kwa himaya na uungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani na utawala wa Saudi Arabia.    

Tags