Mfuko wa UN wa kuwasaidia wakimbizi wa Sudan Kusini wakauka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5827-mfuko_wa_un_wa_kuwasaidia_wakimbizi_wa_sudan_kusini_wakauka
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa unakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kuwasaidia maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini na haswa ambao wamekimbilia nchi jirani ya Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2016 03:49 UTC
  • Mfuko wa UN wa kuwasaidia wakimbizi wa Sudan Kusini wakauka

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa unakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kuwasaidia maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini na haswa ambao wamekimbilia nchi jirani ya Sudan.

Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, Mfuko wa Watoto wa umoja huo UNICEF na Mpango wa Chakula Dunia WFP zimesema kuwa zinakabiliwa na uhaba wa dola milioni 400 za Marekani za kuwashughulia wakimbizi hao.

UNHCR imesema inahitaji dola milioni 105 za Marekani kukidhi mahitaji ya kibinadamu ya wakimbizi hao mwaka huu 2016 huku WFP ikisema kuwa inahitaji dola 181 kwa ajili ya wakimbizi hao katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Zaidi ya wakimbizi laki 6 na 78 elfu wa Sudan Kusini kwa sasa wanapewa hifadhi katika nchi zinazopakana nayo huku laki 2 na elfu 21 kati yao wakiwa wakimbizi katika nchi jirani ya Sudan. Tokea Januari mwaka huu hadi sasa, Sudan imepokea wakimbizi 50 elfu kutoka nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba mwaka 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Mgogoro huo ulianza baada ya Rais Salva Kiir kumfuta kazi makamu wake Riek Machar kwa tuhuma za kupanga njama ya kumpindua mamlakani.

Kwa sasa Machar anasubiriwa kurejea Juba kwa ajili ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na Kiir, kwa mujibu wa makubaliano ya amani ya nchi hiyo.