Bunge la Uturuki laidhinisha kutumwa askari wa nchi hiyo Libya
Bunge la Uturuki limepasisha muswada wa sheria inayoruhusu kutumwa wanajeshi wa nchi hiyo huko Libya.
Muswada huo ulipasishwa jana Alkhamisi katika kikao kisicho cha kawaida cha Bunge la Uturuki. Spika wa Bunge hilo, Mustafa Sentop amesema muswada huo umepasishwa kwa kura 325 za 'Ndio' na 184 za 'Hapana'.
Bunge hilo lililazimika kukatiza likizo yake ya msimu ya kipupwe ili kujadili muswada huo wa sheria inayoruhusu kutumwa askari wa Kituruki nchini Libya kwenda kushirikiana na wanajeshi wa Serikali ya Mapatano ya Kitaifa ya Libya inayotambuliwa na jamii ya kimataifa.
Bunge la Uturuki limechukua uamuzi huo licha ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuonya kuwa, "Hatua ya upande mmoja itakayopelekea kutumwa vikosi ajinabi nchini Libya haitakuwa na tija nyingine ghairi ya kushadidisha mgogoro unaolikumba taifa hilo."
Jeshi la Sarraj limekuwa likibaliana na wapiganaji wa Khalifa Haftar ambao mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2019 walianzisha mashambulizi ya kutaka kuudhibiti mji mkuu, Tripoli.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya 2,000 wakiwemo raia 280 wameuawa jijini Tripoli na wengine wasiopungua 140,000 wamejeruhiwa tangu kuanza mashambulizi hayo ya kundi la wanamgambo wa Haftar, linalojiita jeshi la kitaifa la Libya.