Serikali ya Libya yasimamisha mazungumzo ya amani baada ya Haftar kushambulia bandari
Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya (GNA) inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa haitaendelea kushiriki mkutano wa amani wa UN mjini Geneva, baada ya kukiukwa makubaliano dhaifu ya usitishaji vita.
Katika taarifa ya jana Jumanne, serikali hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj imesema "tunatangaza kusimamisha ushiriki wetu katika mkutano wa kijeshi unaoendelea Geneva hadi pale hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya mvamizi (Haftar) na kukiuka kwake makubaliano ya usitishaji vita kwa muda. Bila usitishaji vita wa kudumu, mazungumzo haya maana. Amani haiwezi kupatikana katika anga ya mashambulizi ya mabomu."
Taarifa ya GNA imesisitiza kuwa, lengo la hujuma hizo za mabomu dhidi ya makazi ya raia, uwanja wa ndege na bandari sambamba na kuzuia kikamilifu uzalishaji wa mafuta ni kuwasababishia migogoro wananchi wote wa Libya. Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya imeongeza kuwa, wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftar baada ya kushindwa kutwaa madaraka kwa mabavu, sasa wanataka kusababisha ukosefu wa uthabiti nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umeendelea kukosoa vikali ukiukwaji wa vikwazo vya siliha viliyowekwa na umoja huo dhidi ya Libya.
Tangazo la Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya limekuja masaa machache baada ya Yaqub al Halwi, Naibu Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya kusema kwamba, nchi nne za Misri, Imarati, Jordan na Russia zinamuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar kwa kuwapatia silaha wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya zikiwemo ndege zisizo na rubani na kuwasimamia moja kwa moja.
Duru za habari zinaarifu kuwa,Saudi Arabia na Imarati pia zimewaajiri na kuwapa mafunzo mamluki kutoka nchi za Sudan na Chad na kuwatuma Libya kulisaidia kundi la Khalifa Haftar linalopigana kudhibiti mji mkuu Tripoli Aprili mwaka jana.