Indhari ya UN kuhusu kubadilika mzozo wa Libya kuwa vita vya kieneo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59492-indhari_ya_un_kuhusu_kubadilika_mzozo_wa_libya_kuwa_vita_vya_kieneo
Licha ya mazungumzo na juhudi za kimataifa katika wiki za hivi karibuni kwa ajili ya kuhitimisha vita nchini Libya, lakini mapigano yamezidi kuongezeka na sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imegeuka kuwa ulingo wa vita vya niaba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2020 20:50 UTC
  • Indhari ya UN kuhusu kubadilika mzozo wa Libya kuwa vita vya kieneo

Licha ya mazungumzo na juhudi za kimataifa katika wiki za hivi karibuni kwa ajili ya kuhitimisha vita nchini Libya, lakini mapigano yamezidi kuongezeka na sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imegeuka kuwa ulingo wa vita vya niaba.

Katika uwanja huo, Umoja wa Mataifa umetahadharisha juu ya uwezekano wa kubadilika mzozo wa nchi hiyo kuwa vita vya kieneo. Kuhusiana na suala hilo, Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa, uwepo wa nchi za kigeni ndani ya Libya unachochea ghasia na mapigano na kuibadili nchi hiyo kuwa ulingo wa vita vya kieneo. Vita nchini Libya vimeshtadi zaidi katika siku za hivi karibuni. Katika mashambulizi ya wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' hapo tarehe 28 Februari dhidi ya uwanja wa ndege wa Tripoli, kuliharibiwa maeneo muhimu na miundombinu ya uwanja huo. Mashambulizi ya wiki za hivi karibuni ya wanamgambo wa Haftar yamepelekea kuharibiwa taasisi nyingi na miundomsingi ya nchi hiyo ikiwemo pia sekta ya mafuta. Mashambulizi nchini humo yameongeze kakatika hali ambayo katika wiki za hivi karibuni kumefanyika juhudi kubwa katika ngazi ya kimataifa kwa ajili ya kuhitimishwa mgogoro ndani ya Libya, zikiwemo juhudi za kuandaa vikao vya mazungumzo nchini Russia na Ujerumani kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi tofauti na pande husika katika mzozo huo.

Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya

Licha ya juhudi hizo na katika hali ambayo ilikuwa imepangwa kupitia vikao hivyo, kuweze kufanyika vikao vya mazungumzo ya amani kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa pande hasimu huko mjini Geneva, Uswisi, pande hizo zilikataa kushiriki vikao hivyo. Hatua ya pande hizo za Libya ya kususia kushiriki mazungumzo ya mjini Geneva, iliufanya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya kutangaza kufeli kwa mazungumzo hayo. Hivi sasa hali nchini Libya inazidi kuwa mbaya siku baada ya nyingine. Kwa sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imegeuka kuwa ulingo wa mizozo ya ndani, uingiliaji na makabiliano ya nchi za kigeni. Katika uga wa kigeni, akthari ya nchi hazifuatilii suala la kufikiwa amani nchini Libya, bali zinahusika katika kuchochea vita kwa njia ya moja kwa moja au aisiyo ya moja kwa moja. Kuhusiana na suala hilo, Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya sambamba na kutangaza kuvunjika mazungumzo ya amani mjini Geneva, amesema kuwa, kuna kundi ambalo halipo tayari kufanya mazungumzo ya kisiasa kwa lengo la kufikiwa amani na kundi jingine pia linatoa mapendekezo yasiyotekelezeka kwa ajili ya kuvuruga juhudi za kutatuliwa kisiasa mgogoro wa Libya. Hivi sasa baadhi ya nchi za eneo na nje ya eneo zimekuwa waungaji mkono wa moja ya pande hasimu nchini Libya. Kiasi kwamba Russia, Saudi Arabia, Imarati, Jordan na Misri zinamuunga mkono Khalifa Haftar ambapo zinafanya juu chini kumpatia jeneri huyo muasi misaada ya aina tofauti ya kilojestiki na kijeshi ili ziweze kufikia maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi nchini Libya. Kwa upande mwingine serikali ya Maridhiano ya Kiataifa nchini Libya pia inaungwa mkono na Uturuki, Qatar, Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi.

Mahasimu wa Libya

Hivi sasa pande mbili za mapigano nchini Libya zinatuhumiana kwa kupokea aina mbalimbali za misaada ya kijeshi kutoka nchi za kigeni. Katika uwanja huo, serikali ya Maridhiano ya Kitaifa imefichua kutumwa shehena ya tani 6200 ya silaha na zana za kijeshi kutoka serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwa Khalifa Haftar katika hali ambayo azimio nambari 1970 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linapiga marufuku kutumwa silaha nchini Libya. Kwa mujibu wa Haftar, askari wengi wa Uturuki wametumwa Libya kwa ajili ya kuiunga mkono serikali ya maridhiano ya kitaifa. Kwa mujibu wa baadhi ya takwimu, katika mapigano ya kusini mwa mji wa Tripoli, hadi sasa zaidi ya askari 16 wa Uturuki wameuawa na wapiganaji wa Khalifa Haftar. Ni kwa kuzingatia mazingira ya sasa, ndipo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya akatahadharisha kuhusu kubadilika Libya kutoka mgogoro wa vita vya ndani na kuwa uwanja wa vita vya kieneo. Kwa mtazamo wake, suala hilo litasababisha hasara isiyoweza kufidika. Inaonekana kwamba pande hasimu nchini Libya zinaamini kuwa vita ndio njia pekee ya utatuzi wa mzozo uliopo nchini humo, huku zikighafilika na ukweli kwamba uingiliaji wa kigeni ndani ya nchi hiyo, si tu kwamba unaiweka hatarini nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, bali pia unaliweka hatarini eneo zima la kaskazini mwa Afrika na kulifanya likumbwe na machafuko na ghasia zisizo na mwisho.