UNICEF: Vita nchini Libya vimekuwa na taathira mbaya mno hasa kwa watoto
(last modified Thu, 05 Mar 2020 08:18:05 GMT )
Mar 05, 2020 08:18 UTC
  • UNICEF: Vita nchini Libya vimekuwa na taathira mbaya mno hasa kwa watoto

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watu wasiopungua 1,800,000 wameathirika vibaya na vita vya ndani nchini humo ambapo 266,000 kati yao ni watoto wadogo.

Ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) imeeleza kuwa, makumi ya watoto wa Libya wameuawa na kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya anga, ufyatuaji risasi, utumiaji wa silaha nzito na nyepesi na kulipuka mada za milipuko katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo inaeleza kuwa, maelfu ya familia nchini Libya zimelazimika kuwa wakimbizi huku miundombinu muhimu ya nchi hiyo ikiharibiwa vibaya.

Hivi karibuni pia Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulitahadharisha kwamba, mashambulio ya kiholela dhidi ya makazi ya raia nchini Libya yameifanya hali ya watoto na raia nchini humo izidi kuwa mbaya.

Ripoti mbalimbali zinabainisha kuwa, roho za mamia ya watoto wa Libya zimepotea kufuatia kushadidi hali ya ukosefu wa usalama katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Baada ya kupinduliwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi huko Libya mwaka 2011, nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani na hivi sasa kuna serikali mbili hasimu, moja ya mashariki na nyingine ya magharibi mwa nchi hiyo ambapo vikosi vya pande hizo mbili vinaendelea kupigana,

Tokea Aprili mwaka jana wakati Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji mkuu Tripoli, watu zaidi ya 1,100 wameuawa, zaidi ya 5700 wamejeruhiwa na zaidi ya 146,000 kuachwa bila makao.