Mar 20, 2020 12:25 UTC
  • Makamanda na wanachama wa Boko Haram wauawa katika hujuma za anga Nigeria

Wizara ya Ulinzi ya Nigeria imethibitisha habari za kuangamizwa makamanda wa ngazi za juu na wanachama kadhaa wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.

Bernard Onyeuko, msemaji wa wizara hiyo amesema leo Ijumaa kuwa, mbali na viongozi na wanachama kadhaa wa genge hilo la ukufurishaji kuuawa, lakini pia jeshi la Nigeria limefanikiwa kusambaratisha ngome za magaidi hao katika mashambulio ya anga huko magharibi mwa mji wa Alinwa katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi karibu na eneo la Ziwa Chad.

Bila kutaja idadi, amesema makamanda na wapiganaji kadhaa wa genge la kigaidi la Daesh katika eneo la Magharibi mwa Afrika (ISWAP) wameangamizwa katika operesheni hiyo ya Jumatano iliyopewa jina la (Operation Decisive Edge), walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kufanya mkutano wao.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria ameongeza kuwa, operesheni hiyo ni sehemu ya operesheni kuu ya Lafiya Dole ya kusambaratisha kikamilifu harakati za Boko Haram katika taifa hilo.

Genge la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram

Haya yanajiri siku chache baada ya Wizara ya Ulinzi ya Niger kutangaza kuwa magaidi 50 wanachama wa kundi la Boko Haram wameangamizwa katika eneo la Toumour katika mkoa wa Diffa, huko kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Magaidi wa kundi la Boko Haram hadi sasa wameua watu wasiopungua elfu 20 katika nchi za Nigeria, Cameroon, Chad na Niger tangu walipoanza hujuma dhidi ya vituo vya serikali, misikiti, vyuo, mashule na makanisa katika eneo la magharibi mwa Afrika mwaka 2009. 

 

Tags