Misri yapongeza hatua ya Machar kurejea Juba kuunda serikali
Serikali ya Misri imepongeza hatua ya Riek Machar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini kurejea mjini Juba kwa ajili ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na hasimu wake wa kisiasa Rais Salva Kiir.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema kuwa, kurejea kwa Machar ni hatua kubwa ya kurejesha amani, usalama na uthabiti katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Taarifa hiyo imetoa wito wa ushirikiano wa nchi za eneo na kimataifa kwa shabaha ya kuhakikisha kuwa nchi hiyo inatekeleza makubaliano ya amani yaliyosainiwa Agosti mwaka jana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Haya yanajiri siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kupongeza hatua hiyo na kusisitiza kuwa inaashiria mwamko na mwanzo mpya wenye matumaini. Herve Ladsous, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na vikosi vya kulinda amani vya umoja huo aliliambia Baraza la Usalama la UN kuwa, "Ni muhimu sana kwa pande husika kutumia fursa hii kuonyesha namna walivyojitolea kutekeleza makubaliano ya amani.”
Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Marekani imewaonya viongozi wa Sudan Kusini kuwa, watakabiliwa na vikwazo ikiwa hawatoheshimu makubaliano ya amani.
Siku ya Jumanne, Machar aliwasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba na kuapishwa kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo katika serikali inayoongozwa na hasimu wake wa muda mrefu, Rais Salva Kiir.