Wanamgambo wa Haftar wafanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu Tripoli
Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya imetangaza kuwa, wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar wamefanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.
Tangazo la serikali hiyo inayoongozwa na Fayez al-Sarraj na ambayo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa linaeleza kuwa, kwa akali wanamgambo hao wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wamerusha maroketi na mizinga 132 dhidi ya mji mkuu Tripoli.
Taarifa za awali zinasema kuwa, watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa kufuatia mashambulio hayo.
Wizara ya Afya ya Libya imetangaza kuwa, jana Ijumaa mashambulio kadhaa yalifanywa na wanamgambo hao watiifu kwa jenerali muasi Khalifa Haftar dhidi ya makazi ya raia mjini Tripoli.
Wanamgambo hao wamekataa kuitikia wito wa jamii ya kimataifa unaotaka kusitishwa mashambulio hayo ili kutoa fursa ya kuchukuliwa hatua za kukabiliana na virusi vya Corona na kuwafikishia huduma za tiba watu walioambukizwa virusi hivyo.
Mapigano yameshadidi na kupamba moto katika siku za hivi karibuni katika viunga vya mji mkuu wa Libya, Tripoli kati ya vikosi vitiifu kwa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa (GNA), inayoungwa mkono na Jamii ya Kimataifa na vya kundi la LNA vinavyoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar.
Umoja wa Mataifa umetoa indhari kuhusu matokeo mabaya ya kuendelea kwa mapigano mjini Tripoli na kutoa wito wa kutaka yasitishwe mara moja.