Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya yaanzisha operesheni ya kukomboa Tarhunah
Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya limeanzisha operesheni kubwa ya kijeshi ya kudhibiti mji wa Tarhunah, ngome kuu iliyiobakia ya askari watiifu wka mbabe wa kivita, jenerali mstaafu Khalifa haftar huko magharibi mwa Libya.
Jeshi la Serikali ya mwafaka wa Kitaifa limetangaza kwamba hadi sasa limeua na kuteka nyara wapiganaji wengi wa haftar na zana nyingi za kivita.
Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) Jenerali Muhammad Qanunu amesema jeshi la serikali hiyo limeua wapiganaji kadhaa wa Jenerali Haftar na kuteka nyara wengine wengi katika mapigano yanayoendelea kwenye mji wa Tarhunah ulioko uumbali wa kilomita 80 kusini mwa Tripoli. Amesema hujuma hiyo ni sehemu ya operesheni iliyopewa jina la "Kimbunga cha Amani" yenye lengo la kukomboa maeneo na miji inayodhibitiwa na wapiganaji wa Khalifa Haftar.
Ndege za kijeshi za Jenerali Haftari zimejibu mashambulizi hayo kwa kushambulia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mitiga mjini Tripoli na viunga vya makazi ya raia vya mji huo.
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya kuendelea kwa mapigano mjini Tripoli na kutoa wito yasitishwe mara moja.