Mafuriko yaua watu 25 mashariki mwa Kongo DR
Kwa akali watu 25 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kiza Muhato, afisa mratibu wa jiji la Uvira, mkoa wa Kivu Kusini aliliambia shirika la habari la Associated Press jana Jumamosi kuwa, mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kwamba shughuli za kusaka miili ya wahanga wa janga hilo zinaendelea.
Amesema janga hilo la kimaumbile limepelekea makumi ya maelfu ya watu kupoteza makazi yao huko mashariki mwa DRC.
Afisa huyo mratibu wa eneo la Uvira, mkoa wa Kivu Kusini amesema nyumba 3,500 zimesombwa na mafuriko hayo, na kupelekea watu 77,790 kuachwa bila makao.

Habari zaidi zinasema kuwa, watu wasiopungua 45 walijeruhiwa vibaya siku ya Ijumaa baada ya mto Mulongwe katika jijini la Uvira kuvunja kingo zake kutokana na mafuriko hayo.
Mathias Gillmann, msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema familia 1,000 zimepoteza makazi yao katika mafuriko hayo, na kwamba UN inashirikiana na maafisa wa serikali katika eneo hilo kuwapa misaada ya dharura waathirika wa janga hilo, hususan maji ya kunywa.