Jeshi la serikali ya Libya ladhibiti ngome kadhaa za kijeshi
Wanajeshi wa serikali inayoongozwa na Fayez al-Sarraj, sambamba na kusonga mbele kuelekea mji wa Tarhunah na kudhibiti moja ya ngome muhimu za wanamgambo wa Khalifa Haftar, wamedhibiti pia ngome kadhaa eneo hilo.
Baada ya wanajeshi wa serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Al-Sarraj kukomboa miji kadhaa ikiwemo ya Sabratah na Surman kutoka mikononi mwa wapiganaji wanaoungwa mkono na Khalifa Haftar wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya', sasa wamesonga mbele kuelekea mji wa Tarhunah. Kwa mujibu wa Mohammad Qanunu, Msemaji wa Jeshi la Serikali ya Fayez Al-Sarraj, wanajeshi wa serikali wamedhibiti ngome kadhaa za kijeshi katika viunga vya mji wa Tarhunah ikiwemo ngome ya Al-Hawatim na muthalath Al-Qaumah ambazo ziko umbali wa karibu kilomita 10 katikati ya mji, na kwamba karibu wanamgambo 20 wa Haftar wameuawa na wengine 102 kutiwa mbaroni.
Katika upande mwingine, ndege za jeshi la Al-Sarraj zimetoa indhari kwa lugha ya Kiarabu kwa wakazi wa Tarhunah juu ya kutosogelea ngome za kijeshi na maghala ya silaha ya Haftar. Wakati huo huo, Muhammad Al-Ghasri, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Libya amesema kuwa, baada ya kutolewa indhari hiyo kwa wakazi wa mji huo na kuwataka kutojiingiza vitani sambamba na kuweka chini silaha zao, imebainika kuwa vita na jenerali muasi Khalifa Haftar havihusishi tu upande wa kijeshi, bali upande wa kijamii pia.