Kubatilisha Khalifa Haftar makubaliano ya Skhirat na kujitangaza kuwa kiongozi wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60662-kubatilisha_khalifa_haftar_makubaliano_ya_skhirat_na_kujitangaza_kuwa_kiongozi_wa_libya
Katika hali ambayo mapigano baina ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa Libya na wanamgambo watiifu kwa Khalifa Hatar yangali yanaendelea, jenerali huyo muasi amechukua hatua ya upande mmoja ya kuvunja makubaliano ya kisiasa ya Skhirat na kujitangaza kuwa kiongozi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 28, 2020 20:18 UTC
  • Kubatilisha Khalifa Haftar makubaliano ya Skhirat na kujitangaza kuwa kiongozi wa Libya

Katika hali ambayo mapigano baina ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa Libya na wanamgambo watiifu kwa Khalifa Hatar yangali yanaendelea, jenerali huyo muasi amechukua hatua ya upande mmoja ya kuvunja makubaliano ya kisiasa ya Skhirat na kujitangaza kuwa kiongozi wa nchi hiyo.

Mbabe huyo wa kivita ambaye hivi karibuni aliwataka Walibya wajitokeze katika mitaa na barabara za nchi hiyo kwa ajili ya kuiangusha Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj, Jumatatu ya juzi tarehe 27 Aprili sambamba na kubatilisha makubaliano ya Skhirat alijitangaza kuwa kiongozi wa Libya. Haftar alisema katika tangazo lake hilo kwamba: Tunatangaza kuyabatilisha makubaliano ya kisiasa yenye kutia shaka ya Skhirat ambayo yameiangamiza Libya na kuitumbukiza katika korongo hatari; na tunachukua majukumu tuliyopatiwa na nyinyi wananchi; kwani sasa sisi ndio tunaostahiki kuongoza.

Makubaliano ya kisiasa baina ya pande mbili hasimu nchini Libya ambayo yameondokea kuwa mashuhuri kwa jina la ‘Makubaliano ya Skhirat’, yalitiwa saini Aprili 17 mwaka 2015 chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa huko katika mji wa Skhirat nchini Morocco. Lengo la makubaliano hayo lilikuwa ni kuhitimisha vita vya ndani nchini Libya. Aidha makubaliano hayo yalisisitiza juu ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa uongozi wa Fayez al-Sarraj.

Wajumbe wakionyesha furaha na mshikamano baada ya kutiliana saini ‘Makubaliano ya Skhirat’, Aprili 17 mwaka 2015  katika mji wa Skhirat nchini Morocco

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa itaongoza kipindi cha mpito hadi kutakapofanyika uchaguzi nchini Libya. Hata hivyo Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya ilianza kukabiliwa na upinzani katika siku za mwanzo tu za makubaliano hayo.

Baada ya kupita muda na kuendelea upinzani na siasa za Khalifa Haftar dhidi ya serikali hiyo, sambamba na uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya Libya, kivitendo Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya ikawa imeshindwa kuyafanyia kazi malengo yaliyoainishwa katika makubaliano ya Skhirat.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kushadidi hitilafu na kuongezeka mapigano nchini Libya, kivitendo kumepelekea nchi hiyo kugawanyika katika kambi mbili za ndani na za nje zinazomuunga mkono Khalifa Haftar na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hali imezidi kuwa mbaya zaidi hasa baada ya kushadidi mashambulio ya Khalifa Haftar na uungaji mkono wa siri na wa dhahiri wa nchi kama Misri, Saudi Arabia, Imarati na baadhi ya nchi za Ulaya kwa jenerali huyo muasi.

Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Libya 

Haftar amekuwa akifanya juhudi za kuudhibiti mji mkuu Tripoli ili achukuea rasmi usukani wa kuiongoza Libya. Hata hivyo kusimama kidete vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa kumemfanya si tu kwamba, ashindwe kufikia lengo lake hilo, bali baada ya kuanza operesheni ya ‘Dhoruba ya Amani’ ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa kumevifanya vikosi vyake vishindwe vibaya na kupoteza maeneo mengi ya kaskazini magharibi mwa Libya ambayo yamekombolewa na vikosi vya serikali ya Tripoli.

Ushindi wa hivi karibuni wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa umevuruga kabisa mahesabu ya Khalifa Haftar ya kuchukua hatamu za uongozi wa Libya na kuwa na uongozi mutlaki kiasi kwamba, serikali ya al-Sarraj inasema kuwa, hatua ya sasa ya Khalifa Haftar ya kuvunja makubaliano ya Skhitar na kujitangaza kuwa kiongozi wa Libya inalenga kuhalalisha kushindwa kwake vibaya katika vita nchini humo.

Katika radiamali yake kwa hatua hiyo ya Haftar, Baraz la Uongozi la Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa limesema kuwa, hatua hiyo ni mapinduzi ambayo siyo ya ghafla. Hatua hiyo ni juhudi za Haftar za kufunika kushindwa kwake.

Mapigano nchini Libya

Kwa hakika mgogoro wa Libya umeingia katika awamu mpya. Hatua ya jenerali Khalifa Haftar haiendani na msingi wowote ule wa kidemokrasia na inakwenda kinyume kabisa na malengo ya wananchi wa Libya waliokuwa nayo baada ya kuondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Inaonekana kuwa uingiliaji wa kigeni nchini Libya umefikia kilele licha ya nara na kaulimbiu zote za kimataifa.

Filihali Libya inapitia kipindi cha mgogoro mkubwa na matatizo chungu nzima. Licha ya kufanyika juhudi zote lakini inaonekana kuwa, hatima ya Libya ni vita ambavyo kidhahiri ni vya ndani. Vita ambavyo havina kabisa maslahi na wananchi wa Libya bali ni vya kupora mali na vyanzo vya utajiri wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kama nishati ya mafuta na kutumia nafasi muhimu ya kijiografia ya nchi hiyo kwa ajili ya kupenya kuelekea katika maeneo mengine ya dunia zikiwemo nchi za Kiafrika; na haya ndio mambo yanayopewa kipaumbele na waungaji mkono wa nyuma ya pazia wa vita vya Libya.