Umoja wa Mataifa wakataa kuitambua serikali ya Libya aliyojiundia Haftar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60667-umoja_wa_mataifa_wakataa_kuitambua_serikali_ya_libya_aliyojiundia_haftar
Umoja wa Mataifa umetangaza msimamo wake kuhusu hatua aliyochukua jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar ya kujitangaza mtawala wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, unayoitambua umoja huo ni Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA) pekee na si mtu mwingine yeyote.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Apr 28, 2020 22:32 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakataa kuitambua serikali ya Libya aliyojiundia Haftar

Umoja wa Mataifa umetangaza msimamo wake kuhusu hatua aliyochukua jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar ya kujitangaza mtawala wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, unayoitambua umoja huo ni Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA) pekee na si mtu mwingine yeyote.

Stephanie Williams, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amelieleza shirika rasmi la habari la Ujerumani kuwa, amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kiongozi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya Fayez al-Sarraj na kubadilishana naye mawazo kuhusu matukio ya karibuni yaliyojiri nchini humo.

Sambamba na kuiunga serikali ya Sarraj kulingana na makubaliano ya Skhirat, Williams amesema: Mabadiliko yoyote ya kisiasa nchini Libya inapasa yafanyike kwa kutumia nyenzo za kidemokrasia.

Viongozi wa mirengo hasimu nchini Libya: Fayez al-Sarraj (kulia) na Khalifa Haftar

Jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) siku ya Jumatatu alijitangaza mtawala mpya wa nchi hiyo katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni na kuyafuta makubaliano ya mwaka 2015 yajulikanayo kama "Makubaliano ya Skhirat". 

Mkataba wa Skhirat ulisainiwa Desemba 2015 katika mji wa Skhirat nchini Morocco baina ya pande mbili zinazopigana nchini Libya mbele ya mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi kadhaa wa nchi za Kiarabu na za Magharibi. Kusainiwa makubaliano ya Skhirat kuliandamana na uundwaji wa Baraza la Uongozi na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA); lakini baada ya kupita muda tangu kusainiwa makubaliano hayo, jenerali Haftar alitangaza kuwa, baraza hilo uongozi na serikali ya mwafaka wa kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj hazina uhalali wa kisheria.../