Russia: Hatulitambui tangazo la serikali ya Haftar nchini Libya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, serikali ya Moscow haikubali utawala wa kujitwika wa kiongozi wa wanamgambo wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' nchini humo.
Sergey Lavrov amesema: "Kama ambavyo hatukuunga mkono taarifa ya hivi karibuni ya Fayez al-Sarraj, Maziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ya kutofanya mazungumzo na Khalifa Haftar, hivi sasa pia tunapinga uamuzi wa Haftar kuhusu mustakbali na maisha ya watu wa Libya." Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa, Moscow haiungi mkono taarifa ya Al-Sarraj wala taarifa ya Haftar nchini Libya ambazo hazisaidii kuiondoa nchi hiyo katika hali ya sasa, kupitia mazungumzo ya umoja wa kitaifa. Lavrov ameashiria matamshi ya Aguila Saleh Issa, Spika wa Bunge la Mashariki mwa Libya aliye karibu na Khalifa Haftar, kuhusu pendekezo lake la kufanyika mazungumzo ya kitaifa kwa lengo la kuundwa taasisi za kiserikali zenye kukubalika na pande hasimu, na kuongeza kuwa, pendekezo hilo limetolewa mara kadhaa, na kuwa la muhimu ni kwa pande hizo kuwa na muelekeo na nia nzuri ya kufanyika mazungumzo hayo.
Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa kundi la wapiganaji wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' Jumatatu iliyopita alitangaza kupitia ujumbe wa televisheni kwamba sasa yeye ndiye mtawala wa Libya na wakati huohuo kufutilia mbali mapatano ya amani ya mwaka 2015 mashuhuri kama Mapatano ya Skhirat. Mapatano ya Skhirat yalitiwa saini mwezi Disemba 2015 katika mji wa jina hilo nchini Morocco kati ya pande mbili hasimu za Libya na kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na wa nchi za Kiarabu na Magharibi.