May 15, 2020 00:28 UTC
  • Magaidi 75 wa Boko Haram waangamizwa kusini mwa Niger

Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza habari ya kuuawa makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika operesheni za jeshi la nchi hiyo huko kusini mashariki mwa nchi.

Taarifa ya wizara hiyo imesema magaidi 75 wa Boko Haram wameuawa katika operesheni mbili tofauti za wanajeshi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, kusini mashariki mwa nchi.

Taarifa hiyo imebanisha kuwa, wanachama 25 wa Boko Haram waliuawa katika operesheni ya Jumatatu katika mji wa Difa, ulioko kusini mwa nchi. 

Wizara ya Ulinzi ya Niger imeongeza katika taarifa hiyo kuwa, magaidi wengine 50 wa genge hilo la kitakfiri waliuawa katika operesheni ya pili katika eneo la Ziwa Chad.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu wasiopungua 20 kuuawa katika mashambulizi yaliyotekelezwa na wabeba silaha wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Boko Haram katika vijiji vya Gadabo, Zibane Koira-Zeno na Zibane-Tegui, magharibi mwa Niger.

Baadhi ya wanachama wa Boko Haram

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram lilianzisha shughuli zake za kigaidi mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria ambapo hadi sasa limepanua wigo wake hadi katika nchi za Niger, Cameroon na kaskazini mwa Chad.

Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, katika muongo mmoja wa shughuli za kundi la Boko Haram nchini Nigeria, zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamekuwa wakimbizi.

 

Tags