Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya: Tunakaribia kupata ushindi mkubwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61079-serikali_ya_mwafaka_wa_kitaifa_libya_tunakaribia_kupata_ushindi_mkubwa
Kiongozi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) Fayez al-Sarraj amesisitiza kuwa vikosi vya serikali yake vinakaribia kupata ushindi mkubwa baada ya kukikomboa kituo cha anga cha al-Watiya kilichoko magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo,Tripoli.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 19, 2020 15:23 UTC
  • Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya: Tunakaribia kupata ushindi mkubwa

Kiongozi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya (GNA) Fayez al-Sarraj amesisitiza kuwa vikosi vya serikali yake vinakaribia kupata ushindi mkubwa baada ya kukikomboa kituo cha anga cha al-Watiya kilichoko magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo,Tripoli.

Jana Jumatatu, Al-Sarraj alitangaza kukombolewa kituo cha kijeshi cha al-Watiya kilichokuwa kikikaliwa na wanamgambo wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar.

Katika taarifa aliyotoa baada ya vikosi vya GNA kukikomboa kituo hicho cha al-Watiya, kiongozi huyo wa Baraza la Uongozi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya alisema: "Kwa fahari na heshima kubwa ninatangaza kukombolewa kituo cha al-Watiya kilichokuwa kimevamiwa na wanamgambo watenda jinai. Ushindi wa leo sio mwisho wa mapambano, bali unatufanya tuzidi kuukaribia ushindi mkubwa wa kuikomboa miji na maeneo na kuutokomeza kikamilifu mpango wa ubeberu na udikteta."

Vikosi vya jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya vimetangaza kuwa: Kukidhibiti kituo hicho cha jeshi la anga kutasaidia kukombolewa kusini mwa Tripoli na Tarhunah kutoka kwenye makucha ya vikosi vya Haftar.

Khalifa Haftar

Kamanda mmoja wa vikosi vya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA) aliyeko katika medani za vita ameripoti kuwa, vikosi vya Haftar vimeondoka katika kituo cha anga cha al-Watiya baada ya shambulio la ardhini lililofanywa na vikosi vya GNA kwa kutumia silaha nzito na za wastani.

Kituo cha anga cha al-Watiya ambacho huko nyuma kilikuwa maarufu kwa jina la Aqaba bin Nafi'i kiko umbali wa kilomita 160 kusini magharibi mwa Tripoli na karibu na maeneo mawili ya al-Jumail na al-Asa magharibi mwa Libya.

Al-Watiya ni moja ya vituo vikubwa zaidi vya jeshi la anga la Libya ambacho ndani yake kuna maghala ya silaha, kituo cha fueli ya ndege, uwanja wa ndege za kivita na kitongoji cha makazi.../