Rais wa Zimbabwe awashambulia Wamagharibi kwa kuingilia masuala ya ndani ya Afrika
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amezishambulia vikali nchi za Magharibi kwa kuendelea kuingilia masuala ya ndani ya mataifa ya Afrika.
Akihutubia taifa jana Jumatatu kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 57 tangu kuasisiwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ambao hii leo unajulikana kama Umoja wa Afrika (AU), Rais Mnangagwa amesema madola ya zamani ya kikoloni hayana mamlaka yoyote ya kuendelea 'kulisomesha' bara Afrika kuhusu masuala ya demokrasia.
Amesisitiza kuwa, nchi za Afrika hii leo zinajivunia demokrasia ilizojitafutia zenyewe kwa jitihada zao. Mnangagwa ameeleza bayana kuwa, bara la Afrika halipaswi kuona aibu kueleza juu ya ukwasi wa turathi zake za kitamaduni, lugha na utambulisho.
Amesema Zimbabwe inaendelea kuteseka na uchumi wake kusambaratika kutokana na uingiliaji wa mambo yake ya ndani, na taifa hilo linaendelea kubanwa kwa vikwazo haramu lilivyowekewa na Wamagharibi kama adhabu ya kuchukua ardhi zake zilizokuwa zimeghusubiwa na walowezi wa Kimagharibi.
Rais wa Zimbabwe ameongeza kuwa, "huku tukiendelea kukumbuka na kusherehekea umoja wa bara letu, sisi hapa Zimbabwe tunaishukuru Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na bara lote la Afrika kwa ujumla kwa kusimama na sisi. Afrika imepinga na kulaani vikwazo dhidi ya Zimbabwe na Sudan, na kuwataka waliochukua hatua hizo haramu na za kihaini kuviondoa vikwazo mara moja bila masharti yoyote."
Mwishoni mwa mwaka uliopita, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat aliunga mkono wito wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wa kutaka Zimbabwe iondolewe bila masharti vikwazo ambavyo imewekewa na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya tokea mwaka 2002.