Bunge la Ethiopia lamruhusu Waziri Mkuu asalie madarakani muda wake ukiisha
Bunge la Ethiopia limepiga kura ya kumuidhinisha Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abiy Ahmed aendelee kuwa madarakani hata baada ya muhula wake wa kuhudumu kisheria utakapomalizika.
Hatua hii inajiri baada ya uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika uliotazamiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu kuakhirisha kutokana na janga la corona.
Shirika la Habari la Ethiopia limeripoti kuwa, "Bunge la Federeseheni (Bunge la Juu) la nchi hii limepasisha uamuzi huo wa kurefusha muda wa mabunge yote hadi pale taasisi za kimataifa za afya zitakapotangaza kuwa janga la corona si tishio tena."
Uamuzi huo jana wa Bunge la Ethiopia umeungwa mkono kwa kura 114 za 'Ndio' na 4 za 'Hapana' huku mjumbe mmoja akisusia kushiriki.
Vyama vya upinzani nchini humo hata hivyo vinasisitiza kuwa, Waziri Mkuu Abiy Ahmed analitumia vibaya janga la corona ili endelee kung'ang'ania madaraka.

Bunge la Juu la Ethiopia limechukua uamuzi huo siku mbili baada ya mwanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini humo Keria Ibrahim wa chama cha TPLF kujiuzulu nafasi yake ya Spika wa Bunge hilo, akilalamikia kuakhirishwa kwa uchaguzi wa nchi hiyo.
Uchaguzi huo wa Bunge unatarajiwa kuwa wa kwanza chini ya uongozi wa Abiy Ahmed, ambapo mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alichukua wadhifa wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Aprili mwaka 2018 na kufanikiwa kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa.