Jun 30, 2020 11:10 UTC
  • Mfalme wa Ubelgiji aiangukia miguuni DRC, aiomba radhi kwa ukoloni

Mfalme Philippe wa Ubelgiji ameiomba radhi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na jinai ambazo nchi hiyo ya Ulaya iliwafanyia Wakongomani kwa muda wa miaka 75 katika kipindi cha ukoloni.

Katika barua aliyomuandikia Rais Felix Tshisekedi wa Kongo DR wakati ambapo taifa hilo la Kiafrika linaadhimisha miaka 60 ya uhuru wake, Mflame Phillipe wa Ubelgiji amesema, "nataka kutoa hisia zangu za ndani za majuto kutokana na makovu ya huko nyuma, uchungu ambao unaendelea kuhuishwa na ubaguzi ambao ungalipo katika jamii zetu."

Haya yanajiri wiki mbili baada ya raia wa DRC kutoa wito wa kuondolewa sanamu la mfalme wa zamani wa Ubelgiji, Leopold II kwenye Bustani ya Rais wa Jamhuri mjini Kinshasa.

Wakongomani walitoa mwito huo baada ya kushuhudiwa maandamano katika nchi mbalimbali duniani za kutaka kuondolewa nembo zote za kikoloni, utumwa na ubaguzi, kufuatia mauaji ya kibaguzi ya raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd mnamo Mei 25.

Mwaka 1885 Mfalme Leopold II alidai kuwa ameinunua Kongo DR na kuifanya milki yake binafsi kwa muda wa miaka 23. Mfalme huyo wa zamani wa Ubelgiji alifanya watu wa Congo kuwa watumwa wake na kuwatumikisha katika kazi za sulubu. Wakoloni hao wa Ubelgiji walikuwa wakikata mikono ya watu walioasi au kukiuka amri yao.

Sanamu la Mfalme Leopold mjini Kinshasa

Utawala wa Mfalme Leopold II unakumbukwa kwa ukatili na jinai za kutisha katika enzi ambapo Kongo DR ilikuwa koloni la Ubelgiji, kati ya mwaka 1885 na 1908. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilijipatia uhuru na kujinasua kutoka kwenye makucha ya Mkoloni Mbelgiji mwaka 1960.

Ikumbukwe kuwa, uhusiano kati ya DRC na mkoloni wake huyo wa zamani Ubelgiji uliingia doa mwaka 2018, kwa sababu za kisiasa wakati Brussels ilipoamua kumwekea mashinikizo rais wa zamani Joseph Kabila asiwanie tena kiti cha urais.

 

Tags