Watu watano Afrika Kusini wauawa katika malumbano ya makundi hasimu kanisani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62157-watu_watano_afrika_kusini_wauawa_katika_malumbano_ya_makundi_hasimu_kanisani
Watu watano wameuawa katika hujuma dhidi ya kanisa nchini Afrika Kusini kusini mwa mji wa Johannesburg. Katika tukio hilo la Jumamosi, washambuliaji hao wenye silaha pia waliwachukua mateka watu kadhaa ambao wamenusuriwa katika oparesheni ya polisi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 12, 2020 08:45 UTC
  • Watu watano Afrika Kusini wauawa katika malumbano ya makundi hasimu kanisani

Watu watano wameuawa katika hujuma dhidi ya kanisa nchini Afrika Kusini kusini mwa mji wa Johannesburg. Katika tukio hilo la Jumamosi, washambuliaji hao wenye silaha pia waliwachukua mateka watu kadhaa ambao wamenusuriwa katika oparesheni ya polisi.

Msemaji wa Polisi Vishnu Naidoo amesema wamewakamata watu 40 na kunasa silaha 40 ambazo zilitumika katika hujuma dhidi ya kanisa linalojulikana kama International Pentecost Holiness Church katika mji wa Zuurbekom mkoani Gauteng.

Taarifa zinasema chanzo cha hujuma hiyo ni malumbano ya kuwania madaraka katika kanisa hilo baina ya makundi mawili hasimu.

Kanisa hili limetajwa kuwa kubwa zaidi, na pengine tajiri zaidi, Afrika Kusini.

Kamishna wa Polisi Afrika Kusini Khehla John Sitole amesema hatua ya polisi kufika katika eneo hilo haraka imezuia umwagikaji mkubwa wa damu ambao ungejiri katika kanisa hilo.

Maafisa wa polisi Afrika Kusini

Kati ya waliokamatwa kwa kuhusika na hujuma hiyo kanisani ni maafisa wa polisi, maafisa wa jeshi na pia askari wa magereza.

Gazeti la Sowetan limeandika kuwa matatizo yaliibuka katika kanisa hilo baada ya kufariki kiongozi wake, Glayton Modise mnamo Februari 2016.