Watu 60 wauawa Darfur, Sudan, waziri mkuu atuma wanajeshi
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 60 wameuawa katika mapigano mapya ambayo yamejiri katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema watu hao wameuawa katika hujuma ya wanamgambo wenye silaha wasiojulikana dhidi ya kijiji kimoja kusini mwa Darfur. Taarifa zinasema miongoni mwa waliouawa ni watoto.
Kufuatia mauaji hayo, Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok amesema wanajeshi watatumwa katika eneo la Darfur kuwalinda raia wakati wa msimu huu wa kilimo.
Hamdok amesema maafisa wa usalama kutoka vikosi kadhaa watatumwa katika majimbo matano ya Darfur kwa lengo la kuwalinda raia
Tangu mwaka 2003, jimbo la Darfur limekumbwa na machafuko na mapigano ya silaha huku makabila ya eneo hilo yakilalamika kuwa serikali imewabagua.

Rais Omar el Bashir aliyeondoelewa madarakani mwaka jana alianzisha oparesheni dhidi ya watu wa Darfur na kupelekea watu wasiopungua 300,000 kuuawa na wengine milioni 2.5 kuachwa bila makao.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeshatoa waranti wa kukamatwa Al Bashir kutokana na jinai za kivita za utawala wake huko Darfur.
Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa zinaendesha operesheni ya kulinda amani katika jimbo hilo chini ya mwavuli wa kikosi cha UNAMID.