Msumbuji yachukua uwenyekiti wa SADC
(last modified Tue, 18 Aug 2020 03:37:55 GMT )
Aug 18, 2020 03:37 UTC
  • Msumbuji yachukua uwenyekiti wa SADC

Tanzania imekabidhi Msumbiji uwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC huku jumuiya hiyo ikiadhimisha miaka 40 tangu kuasisiwa kwake.

Wakati akikabidhi uwenyekiti huo jana Jumatatu, Rais wa Tanzania John Magufuli ameipongeza jamii ya kimataifa kwa kulegeza vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa nchi ya Zimbabwe mwaka 2000.

Akihutubia mkutano huo wa 40 wa Jumuiya hiyo ambao ulifanyika kwa njia ya video akiwa katika ikulu ya Chamwino katika mji mkuu wa Tanzania Dodoma, Rais Magufuli aliongeza kuwa baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha uenyekiti ni pamoja na Kiswahili kufanywa kuwa lugha ya nne rasmi katika Jumuiya hiyo.

Rais Magufuli pia alitoa wito kwa mataifa yaliyoendelea kuweka mpango maalumu kwa kuyasamehe madeni mataifa ya dunia ya tatu ili yajikwamue na janga la COVID-19.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi

 

Mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya SADC umefanyika katika mazingira tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. Kutokana na janga la Covid19, viongozi wa SADC hawakuweza kukutana sehemu moja, bali washiriki wamekutana kwa njia ya video. Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo kwa sasa ni Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi.

Msumbuji inachukua uwenyekiti wa SADC wakati ikiwa inakabiliwa na mashambulizi ya waasi wanaofungama na ISIS katika eneo lenye utajiri wa gesi kaskazini mwa nchi hiyo.