Wanajeshi waliofanya mapinduzi Mali wamuachia huru Rais Keita
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63071-wanajeshi_waliofanya_mapinduzi_mali_wamuachia_huru_rais_keita
Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali wametangaza habari ya kumuachia huru Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo, ambaye amekuwa akizuiliwa tokea tarehe 18 mwezi huu.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 27, 2020 21:54 UTC
  • Wanajeshi waliofanya mapinduzi Mali wamuachia huru Rais Keita

Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali wametangaza habari ya kumuachia huru Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo, ambaye amekuwa akizuiliwa tokea tarehe 18 mwezi huu.

Viongozi hao chini ya Kamati ya Kitaifa ya Uokovu wa Wananchi (CNSP) walitangaza hayo jana Alkamisi katika ujumbe waliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Taarifa ya wanajeshi hao wafanya mapinduzi imesema: Tunawataarifu wananchi na jamii ya kimataifa kuwa Rais Ibrahim Boubacar Keita ameachiwa huru na hivi sasa yuko katika makazi yake.

Kadhalika Djibrila Maiga, msemaji wa Kamati ya Kitaifa ya Uokovu wa Wananchi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Rais IBK (Ibrahim Boubacar Keita) yuko huru kutembea, hivi sasa yuko nyumbani kwake."

Wanajeshi walioongoza mapinduzi ya Mali na wajumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas)

Familia ya Keita mwenye umri wa miaka 75 imethibitisha habari hizo za kuachiwa huru rais huyo ambaye ameiongoza Mali tokea mwaka 2013, na kwamba hivi sasa yuko katika makazi yake katika wilaya ya Sebenikoro katika mji mkuu Bamako.

Kabla ya kumuachia huru Keita, viongozi wa mapinduzi ya kijeshi huko Mali waliuambia ujumbe wa wapatanishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) kuwa wanataka kusalia madarakani kwa miaka mitatu ya kipindi cha mpito kabla ya kuitishwa uchaguzi.