Rais Conde (82) wa Guinea kugombea muhula wa tatu wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63156-rais_conde_(82)_wa_guinea_kugombea_muhula_wa_tatu_wa_urais
Rais Alpha Conde wa Guinea amekubali uteuzi wa chama chake wa kugombea muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2020 03:16 UTC
  • Rais Conde (82) wa Guinea kugombea muhula wa tatu wa urais

Rais Alpha Conde wa Guinea amekubali uteuzi wa chama chake wa kugombea muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika taarifa, chama tawala cha Rally of the Guinean People (RPG) kimesema, "tuna furaha kuwatangazia wananchi wa Guinea kuwa Rais Alpha Conde amekubali ombi letu la kumtaka agombee urais kupitia chama hiki katika uchaguzi wa Oktoba 18. Mgombea wetu wa urais atakuwa Conde." 

Vyama vya upinzani nchini humo vinasisitiza kuwa, ni kinyume cha katiba kwa Conde kuwania muhula wa tatu kwa kuitumia vibaya katiba mpya ya nchi hiyo.

Mwezi Machi mwaka huu, Tume ya Uchaguzi nchini humo ilitangaza kuwa asilimia 92 ya wapigakura wameunga mkono mabadiliko ya katiba katika kura ya maoni ambayo upinzani unasema kuwa ilimpa Rais Alpha Conde 'kibali' cha kuendelea kutawala kwa miaka mingine 12.

Machafuko yanashuhudia nchini Guinea Conakry tokea Oktoba 2019

Katiba mpya ya Guinea imeweka kikomo cha mihula miwili ya miaka sita, badala ya miaka mitano ya sasa, lakini inaelelekea kuwa Conde ameamua kuitumia katiba hiyo kuanzisha awamu mpya ya muhula wa urais wake.

Watu wasiopungua 30 wameuawa tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita katika maandamano ya upinzani ya kupinga mabadiliko hayo ya katiba.