Wahudumu wa afya waandamana Afrika Kusini, watishia kugoma
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63204-wahudumu_wa_afya_waandamana_afrika_kusini_watishia_kugoma
Wahudumu wa afya nchini Afrika Kusini wamefanya maandamano katika miji ya Pretoria na Cape Town, kulalamikia mazingira magumu ya kufanyia kazi, huku wakiitaka serikali ikabiliane na ufisadi unaoshuhudiwa katika uagizaji wa mavazi maalumu na suhula za kupambana na ugonjwa wa Covid-19.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2020 22:07 UTC
  • Wahudumu wa afya waandamana Afrika Kusini, watishia kugoma

Wahudumu wa afya nchini Afrika Kusini wamefanya maandamano katika miji ya Pretoria na Cape Town, kulalamikia mazingira magumu ya kufanyia kazi, huku wakiitaka serikali ikabiliane na ufisadi unaoshuhudiwa katika uagizaji wa mavazi maalumu na suhula za kupambana na ugonjwa wa Covid-19.

Katika maandamano hayo ya jana Alkhamisi, wafanyakazi hao wa sekta ya afya nchini Afrika Kusini walisema serikali imeshindwa kushughulikia matakwa yao hususan wakati huu wa janga la corona, licha ya wao kuhatarisha maisha yao wakiwahudumia wananchi.

Muungano wa Kitaifa wa Wafanyakazi wa Afya nchini Afrikia Kusini umetishia kuwa, iwapo serikali itaendelea kupuuza kilio chao, hawatakuwa na chaguo jingine ghairi ya kuwaagiza wanachama wake wapatao laki mbili kuanza mgomo wa kitaifa kuanzia Septemba 10.

Kiongozi wa muungano huo, Zola Saphetha ameitaka serikali ya Pretoria iwape 'marupurupu ya kuhatarisha maisha' wafanyakazi wa sekta ya afya ambao wapo katika mstari wa mbele wa kukabiliana na maradhi ya Covid-19. 

Afrika Kusini hivi karibuni imeshuhudia kupungua kwa kesi za corona, licha ya kuongeza kiwango cha vipimo

Takwimu za Wizara ya Afya ya Afrika Kusini zinaonyesha kuwa, tangu tarehe 5 Machi wakati nchi hiyo ilipotangaza mgonjwa wa kwanza wa corona, madaktari na wauguzi 240 wamefariki dunia kutokana na virusi hivyo.

Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kufikia sasa imerekodi kesi zaidi ya 630,595 za Covid-19, idadi ya juu zaidi barani Afrika, mbali na vifo zaidi ya 14,300. Hata hivyo nchi hiyo imeshuhudia kupungua kwa kiasi kikubwa kwa maambukizi ya corona, licha ya kuongeza idadi ya vipimo vya ugonjwa huo.