30 wauawa katika mapigano baina ya al-Shabaab na wanakijiji Somalia
(last modified Sun, 06 Sep 2020 07:35:26 GMT )
Sep 06, 2020 07:35 UTC
  • 30 wauawa katika mapigano baina ya al-Shabaab na wanakijiji Somalia

Makumi ya watu wameuawa katika makabiliano makali baina ya wanamgambo wa al-Shabaab na wanakijiji katikati mwa Somalia.

Osman Isse Nur, msemaji wa serikali ya kieneo ya Galmudug, katikati mwa Somalia amesema watu 30 wakiwemo wanachama 16 wa al-Shabaab wameuawa katika mapigano hayo. Nur alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, makabaliano hayo yalianza baada ya wakazi wa kijiji cha Shabeelow kujizatiti kwa silaha na kukabiliana na wanamagambo wa al-Shabaab waliowavamia kwa lengo la kuiba mifugo wao.

Msemaji wa serikali ya kieneo ya Galmudug ameeleza bayana kuwa, "wanakijiji waliamua kubeba silaha na kupambana na magaidi kwa lengo la kuzuia mifugo wao wasiibiwe."

Abdi Siyaad, kiongozi wa kijamii wa eneo hilo amesema wanakijiji 14 waliuawa katika mapigano hayo ya Ijumaa na kwamba majeruhi wamelazwa katika hospitali moja mjini Galkayo.

Wanachama wa al-Shabaab wanaowahangaisha raia na maafisa usalama Somalia

Ameitaka serikali ya Somalia kuwapa wanavijiji silaha ili wajihami na kujilinda kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanachama wa al-Shabaab.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Tags