Sep 08, 2020 07:49 UTC
  • Watu 10 wauawa katika shambulizi la Boko Haram, Maiduguri Nigeria

Watu wasiopungua 10 wameuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, raia hao waliuawa baada ya wanachama wa Boko Haram kuvamia vijiji vitatu vilivyoko viungani mwa mji wa Maiduguri, makao makuu ya mkoa wa Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.

Habari zaidi zinasema kuwa, makumi ya watu wengine wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya juzi Jumapili ya Boko Haram.

Mapema mwezi uliopita wa Agosti, askari 25 waliuawa katika shambulio la kuvizia lililofanywa na kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji huko kaskazini mwa Nigeria.

Wanachama wa genge la kigaidi la Boko Haram

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lilibeba silaha na kuanzisha uasi mwaka 2009 kwa lengo la kuasisi utawala eti wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo mbali na ndani ya nchi hiyo, limepanua wigo wa mashambulio yake katika nchi jirani pia za Niger, Chad na Cameroon.

Zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika nchi hizo nne za magharibi mwa Afrika na zaidi ya wengine milioni mbili wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao.

Tags