UNICEF yazitaka nchi za mashariki na kusini mwa Afrika zifungue shule
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umezitaka serikali za nchi za mashariki na kusini mwa Afrika kufungua shule haraka iwezekanavyo sambamba na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa salama wanaporejea shuleni.
Mohamed Malick Fall, Mkurugenzi wa UNICEF katika kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika alitoa mwito huo jana Jumanne na kubainisha kuwa, "miezi saba ndani ya janga la corona, lazima tuwe wawazi kuhusu uzito wa mgogoro huu. Tupo katika hatari ya kupoteza kizazi."
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, "tumeshuhudia kufungwa kwa masomo, kuongezeka ghasia na wototo kufanyishwa kazi za sulubu, ndoa na mimba za mapema pamoja ukosefu wa lishe."
Maambukizi ya virusi vya corona kote duniani na kutokuwepo chanjo na dawa mujarabu ya kutibu ugonjwa wa COVID-19 kumezilazimisha nchi mbalimbali kuchukua hatua za dharura zinazohusiana na masuala ya afya ikiwa ni pamoja na kufungwa shule na masomo.

Mkurugenzi wa UNICEF katika kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika ameeleza bayana kuwa, janga la corona limewakatizia masomo watoto milioni 65 katika eneo hilo, na kwamba mamilioni miongoni mwao walikuwa wakitegemea mlo mmoja wenye virutubishi wanaopewa shuleni.
Kwa mujibu wa UNICEF, thuluthi moja ya watoto wanaokwenda shule duniani yaani karibu watoto milioni 500 hawakuweza kupata elimu kwa njia ya mbali (intaneti) katika kipindi cha kufungwa shule kutokana na maambukizi ya corona. Ripoti ya UNICEF imesema kuwa, katika kilele cha utekelezaji wa sheria kali za kuzuia watu kutoka nje kieneo na kitaifa kote duniani, watoto bilioni 1.5 wenye umri wa kwenda shule wameathiriwa kutokana na kufungwa shule na vituo vya elimu.