Genge la wabeba silaha lafanya tena mashambulio na kuua 12 Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63987-genge_la_wabeba_silaha_lafanya_tena_mashambulio_na_kuua_12_ethiopia
Kwa akali watu 12 wameuawa katika shambulizi la wanamgambo waliobeba silaha katika eneo la Benishangul-Gumuz, magharibi mwa Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 13, 2020 04:10 UTC
  • Genge la wabeba silaha lafanya tena mashambulio na kuua 12 Ethiopia

Kwa akali watu 12 wameuawa katika shambulizi la wanamgambo waliobeba silaha katika eneo la Benishangul-Gumuz, magharibi mwa Ethiopia.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Gashu Dugaz, Mkuu wa Taasisi ya Amani na Usalama ya eneo la Benishangul-Gumuz amesema watu hao waliuawa jana Jumatatu, baada ya wanamgambo waliojizatiti kwa silaha kushambulia kijiji kimoja katika manispaa ya Mandura eneo la Metekel.

Ameongeza kuwa, mtu mwingine alijeruhiwa katika hujuma hiyo na anaendelea kutibiwa katika zahanati iliyoko karibu na eneo la tukio hilo. Amesema washukiwa kadhaa wa hujuma hiyo wametiwa mbaroni.

Alkhamisi iliyopita, genge hilo la wanamgambo wanaobeba silaha lilivamia eneo la Metekel katika jimbo la Benishangul-Gumuz, magharibi mwa Ethiopia na kuua watu wengine 14 akiwemo raia mmoja wa kigeni.

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia mwenye azma ya kuleta mageuzi nchini kwake

Kadhalika watu wasiopungua 30 waliuawa katika mashambulizi ya wanamgambo hao katika eneo la Benishangul-Gumuz, mwezi uliopita. Miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi hayo yaliyofanyika baina ya Septemba 6 na 13 ni wanawake na watoto wadogo.

Serikali ya Addis Ababa inasisitiza kuwa, wanaofanya mashambulizi ya aina hii dhidi ya raia wasio na hatia ni katika makundi yanayotaka kukwamisha safari ya mageuzi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.