Kauli ya Mufti wa Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64047-kauli_ya_mufti_wa_tanzania_kuelekea_uchaguzi_mkuu_wa_oktoba_28
Sheikh mkuu na Mufti wa Tanzania Abubakari Zubeir amewataka watanzania kuhakikisha wanailinda amani ya nchi wakati huu ambapo taifa linaelekea kufanya uchaguzi mkuu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 16, 2020 07:28 UTC
  • Kauli ya Mufti wa Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28

Sheikh mkuu na Mufti wa Tanzania Abubakari Zubeir amewataka watanzania kuhakikisha wanailinda amani ya nchi wakati huu ambapo taifa linaelekea kufanya uchaguzi mkuu.

Sheikh mkuu alitoa wito huo jana Alkhamisi jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa ujumbe wa Mufti kuelekea uchaguzi mkuu.

Amesema: Tusitumike na watu wengine kuivuruga amani yetu ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia, hii ni tunu ya Watanzania wote bila ya kujali dini zao na makabila yao. 

Uchaguzi mkuu wa Tanzania unatazamiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba huku kukiwepo na malalamiko makubwa ya vyama vya upinzani dhidi ya utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC imemfungia mgombea wa urais wa chama kikuu cha upinzani visiwani humo cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad kufanya kampeni kwa muda wa siku tano kuanzia leo Ijumaa, kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za uchaguzi.

Maalim Seif katika kikao na waandishi wa habari huko nyuma

Kamati hiyo imechukua hatua hiyo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake na Chama cha Demokrasia Makini kikikadai kuwa Maalim Seif amewashawishi watu wapige kura Oktoba 27.

Aidha mapema mwezi huu, Kamati ya Maadili ya Kitaifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) ilimsimamisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kufanya kampeni kwa muda wa siku saba, kwa tuhuma hizo hizo za kukiuka kanuni na taratibu za uchaguzi.