Waziri wa afya wa Afrika Kusini aambukizwa corona
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64107-waziri_wa_afya_wa_afrika_kusini_aambukizwa_corona
Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Daktari Zweli Mkhize jana alitoa taarifa akithibitisha kuwa, yeye na mke wake wameambukizwa virusi vya COVID-19.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 19, 2020 04:24 UTC
  • Waziri wa afya wa Afrika Kusini aambukizwa corona

Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Daktari Zweli Mkhize jana alitoa taarifa akithibitisha kuwa, yeye na mke wake wameambukizwa virusi vya COVID-19.

Mkhize amesema hivi sasa yeye na mke wake wamejiweka karantini nyumbani, lakini hakubainisha namna alivyoambukizwa virusi hivyo.

Waziri Mkhize amewataka watu waliokutana naye katika siku kadhaa zilizopita kujiweka karantini, vilevile amewahimiza wananchi wa Afrika Kusini waendelee kufuata kanuni za kukabiliana na COVID-19, kama vile kuvaa barakoa kwenye maeneo ya umma, na kudumisha umbali wanapokutana pamoja na kunawa mikono mara kwa mara.

Aidha ametoa wito kwa watu wa Afrika Kusini kuendelea kuchukua tahadhari kwani wimbi la pili la corona ni hatari. 

Siku ya Jumapili, Wizara ya Afya ya Afrika Kusini ilitangaza kuwa hadi sasa watu 703 793 wameambukizwa corona nchini humo na waliopona ni  634 543 au asilimia 90% ya wote walioambukizwa. Waliopoteza maisha kutokana na corona nchini humo hadi sasa ni 18,400.

Wakati huo huo,  kituo cha kudhibiti maradhi cha Ulaya kimesema hadi sasa zaidi ya watu 200,000 wamefariki ndani ya Umoja wa Ulaya na nchi washirika kutokana na virusi vya corona. 

Takwimu hizo za hivi karibuni kutoka kwenye kituo hicho zimeonyesha kuwa karibu watu milioni 4.8 wameambukizwa na jumla ya watu 200,587 wamefariki dunia. Vifo vingi zaidi vimetokea Uingereza, Italia, Uhispania na Ufaransa.