May 05, 2016 02:46 UTC
  • Wabunge wa Afrika Kusini watandikana juu ya hotuba ya Zuma

Bunge la Afrika Kusini jana Jumatano liligeuka na kuwa ukumbi wa mieleka huku wabunge wa upinzani wakizusha fujo kuzuia hotuba ya Rais Jacob Zuma juu ya bajeti.

Maafisa wa usalama wa bunge waliokuwa wamevalia nguo za kawaida walilazimika kuingilia kati na kuwatoa nje wabunge wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters kinachoongozwa na Julius Malema, waliokuwa wakipiga makelele na kusema kuwa hawamtambui Zuma kama rais wa nchi.

Floyd Shivambu, Naibu Rais wa chama hicho aliliambia bunge hilo chini ya kiwingu cha vurumai kuwa: "Hatuwezi kumruhusu rais anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi kuhutubia taifa kana kwamba hakuna chochote kilichofanyika."

Hata hivyo utulivu ulirejea bungeni baada ya kuondolewa wanasiasa wapatao 10 wa upinzani na kisha Rais Jacob Zuma akalihutubia taifa juu ya bajeti ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Wapinzani nchini Afrika Kusini wanamtuhumu Zuma kuwa ni kiongozi fisadi, haswa baada ya Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo kumpata na hatia ya kukiuka katiba na kumuagiza kulipa sehemu ya fedha zilizotumiwa katika ukarabati wa nyumba yake binafsi katika eneo la KwaZulu Natal, mradi ambao uligharimu zaidi ya dola milioni 16 za Marekani. Hata hivyo Rais Zuma alinusurika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni kufuatia kashfa hiyo.

Tags