UN: Ahadi za kurejesha amani CAR zitimizwe kikamilifu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64366-un_ahadi_za_kurejesha_amani_car_zitimizwe_kikamilifu
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia operesheni za kulinda amani Jean-Pierre Lacroix amesema ahadi za kurejesha amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) zinapaswa kutimizwa kikamilifu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 01, 2020 07:55 UTC
  • UN: Ahadi za kurejesha amani CAR zitimizwe kikamilifu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia operesheni za kulinda amani Jean-Pierre Lacroix amesema ahadi za kurejesha amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) zinapaswa kutimizwa kikamilifu.

Ameyasema hayo baada ya kukamilisha ziara yake nchini humo akiwa ameandamana na Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui na Rais wa Tume ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika ya Kati, Balozi Gilberto da Piedade Veríssimo.

Ujumbe huo ulikutana na Rais wa Jamhuri, viongozi wa kidini, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na makundi vyenye silaha. Utekelezaji wa makubaliano ya amani ilikuwa moja ya mada kuu ya ziara hiyo.

Makundi aliyotia saini mkataba wa amani yameelezea kutoridhika kwao mara kadhaa. Siku mbili zilizopita, makundi hayo yalitoa hati nyingine inayoelezea kile wanachoamini kinazuia utekelezaji wa mkataba huo amani, kutofanya kazi kwa vyombo vya utekelezaji, uamuzi wa upande mmoja, viongozi na wawakilishi wa makundi yenye silaha wanaolengwa au kudharauliwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Jean-Pierre Lacroix anakiri kuwa kumekuwepo ucheleweshaji katika baadhi ya mambo yaliyoafikiwa, hasa kuundwa kwa vitengo maalumu vya usalama wa pamoja, ambavyo vinapaswa kuundwa kwa sehemu moja na wapiganaji wa zamani na vikosi vya ulinzi na usalama, kulingana na mkataba wa amani. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia operesheni za kulinda amani Jean-Pierre Lacroix amesema kuwa ahadi zilizotolewa bado zinahitaji kutimizwa kikamilifu.

Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé.

Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu. 

Watu zaidi ya 400,000, wengi wakiwa ni Waislamu wamelazimika kukimbia makazi yao na wengine milioni 2.7, au nusu ya watu wote CAR wanahitaji msaada kutokana na machafuko na mapigano ya ndani. 

Mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu yanasema kuwa, hali ya maisha nchini humo ni mbaya mno na yanasisitiza juu yya udharura wa kuchukuliwa hatua za kukomesha machafuko katika nchi hiyo.