Makumi wauawa katika shambulio la wabeba silaha Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64400-makumi_wauawa_katika_shambulio_la_wabeba_silaha_ethiopia
Makumi ya watu wameuawa katika shambulizi la wanamgambo waliobeba silaha magharibi mwa Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 03, 2020 03:39 UTC
  • Makumi wauawa katika shambulio la wabeba silaha Ethiopia

Makumi ya watu wameuawa katika shambulizi la wanamgambo waliobeba silaha magharibi mwa Ethiopia.

Elias Umeta, afisa wa serikali katika eneo la Oromiya aliliambia shirika la habari la Reuters jana Jumatatu kuwa, watu 32 wameuawa katika shambulio la Jumapili la wanamgambo wa OLF Shane katika kijiji cha Wollega, magharibi mwa nchi.

Amesema mbali na kufanya mauaji hayo, genge hilo lilichoma moto pia nyumba zaidi ya 20, huku watu kati ya 700 na 750 wakilazimika kuyakimbia makazi yao katika eneo hilo wakihofia maisha yao.

Genge la OLF Shane lilijitenga na chama cha kisiasa cha Oromo Liberation Front (OLF), ambacho viongozi wake walikua wakiishi uhamishoni kwa miaka mingi, kabla ya kuruhusiwa kurejea nchini baada ya Waziri Mkuu, Abiy Ahmed kuchukua hatamu za uongozi mwaka 2018.

Wanamgambo wanaobeba silaha Ethiopia

Mwezi uliopita, watu wengine 26 waliuawa katika mashambulizi mawili ya wabeba silaha katika eneo la Benishangul-Gumuz, magharibi mwa Ethiopia. Kadhalika watu wasiopungua 30 waliuawa katika mashambulizi ya wanamgambo hao katika eneo hilo hilo la Benishangul-Gumuz, mwezi mmoja kabla ya hapo.

Serikali ya Addis Ababa inasisitiza kuwa, wanaofanya mashambulizi ya aina hii dhidi ya raia wasio na hatia ni katika makundi yanayotaka kukwamisha safari ya mageuzi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.