Wapinzani wa Afrika Kusini wasusia kikao cha bunge
Wabunge wa vyama vya upinzani jana Alkhamisi walikataa kuhudhuria kikao cha bunge. Siku ya Jumatano wabunge wa chama cha Economic Freedom Fighters walifukuzwa bungeni kutokana na kuvuruga shughuli za bunge.
Kikao hicho kilikuwa kimeitishwa kwa ajili ya kusikiliza hotuba ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo na vilevile kupitisha bajeti ya serikali. Wabunge wa upinzani ambao walikusudia kutomruhusu Rais Zuma ahutubie bunge walizua vurugu baada ya kukabiliwa na wenzao wa chama tawala cha ANC na hatimaye kufukuzwa bungeni. Licha ya vurugu hiyo kuendelea kwa muda wa nusu saa lakini baadaye Rais Zuma alitoa hotuba yake bila tatizo wala mvutano wowote. Kufukuzwa kwa wabunge hao kulipelekea wabunge wa vyama vya upinzani vikiwemo vya United Democratic Movement, Pan Africanist Congress na National Freedom Party kususia kikao cha bunge siku ya Alkhamisi. Akihutubia umati mkubwa wa watu huko Pretoria mji mkuu wa kisiasa wa Afrika Kusini wiki iliyopita, Rais Jacob Zuma alisema hataruhusu nchi hiyo irejee kwenye kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi. Huku akitahadharisha dhidi ya kuenea ghasia na machafuko nchini humo, Rais Zuma alisema kuwa kuna watu wanaotaka kuvuruga usalama na kuzua ghasia za kisiasa nchini na kuonya kuwa serikali haitaruhusu jambo hilo kutokea na kwamba itakabiliana vilivyo na watu wanaotaka kuirejesha nchi hiyo katika kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi. Wanaharakati wa kisiasa na wapinzani wa Zuma wanaamini kwamba serikali ya hivi sasa ya Afrika Kusini haina uwezo wa kuongoza nchi na kumtuhumu Rais Zuma kuwa ndiye muhusika mkuu wa kuenea ufisadi na vurugu nchini humo, tuhuma ambazo zinapingwa vikali na chama tawala. Mwezi uliopita wa Aprili, Julius Malema kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters alionya kuwa atatumia nguvu na ikilazimu silaha kumuondoa Zuma madarakani. Malema ni kiongozi wa zamani wa tawi la vijana la chama tawala cha ANC ambaye aling'olewa madarakai kutokana na hitilafu zilizojitokeza baina yake na viongozi wa chama hicho.
Malema na wanachama wengine wa ANC na vilevile shakhsia wengine mashuhuri wa Afrika Kusini wamemtaka Jacob Zuma ajiuzulu lakini chama hicho kinapinga vikali suala hilo na kuendelea kumtetea. Kabla ya hapo chama cha United Democratic Movement kilikuwa kimeasilisha bungeni mswada wa kutokuwa na imani na Rais Zuma lakini ulipingwa na wabunge 233 dhidi ya 143 walioupigia kura ya ndio. Baada ya kushindwa mswada huo Julius Malema alitishia kuiondoa madarakani kwa nguvu na kwa kutumai silaha serikali ya Jacob Zuma. Alidai kwamba wapinzani hawaliogopi jeshi na kwamba watatumia vita na mapambano ya silaha kufikia lengo lao. Tokea aingie madarakani hapo mwaka 2009 hadi sasa Zuma amekabiliwa mara kadhaa na kura ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa wapinzani kutokana na kashfa kadhaa za matumizi mabaya ya fedha za umma. Kuhusu suala hilo Zuma anawatuhumu wapinzani wake kuwa wanataka kutumia kisingizio hicho kurejesha nchini humo utawala wa zamani wa ubaguzi wa rangi. Anawatuhumu kuwa wanataka kuwa na nafasi na fursa maalumu kinyume na hali ya maisha ya wananchi waliowengi nchini humo ilihali wao sio wawakilishi halisi wa wananchi wala serikali ya nchi hiyo.