Matokeo ya kuendelea kuwepo kijeshi Ufaransa barani Afrika
(last modified Sun, 03 Jan 2021 12:23:21 GMT )
Jan 03, 2021 12:23 UTC
  • Matokeo ya kuendelea kuwepo kijeshi Ufaransa barani Afrika

Uwepo wa kijeshi wa Ufaransa katika maeneo mbalimbali barani Afrika ungali unaendelea.

Katika fremu hiyo na sambamba na kuanza mwaka huu mpya wa 2021 Miladia, Jean Castex, Waziri Mkuu wa Ufaransa amefanya safari nchini Chad kwa lengo la kuonana na wanajeshi wa nchi yake waliopo katika kambi za kijeshi za kistratejia za Paris katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Baada ya kukutana na wanajeshi wa Ufaransa katika kambi za kijeshi zilizoko katika mji mkuu N'Djamena akiwa pamoja na Florence Parly Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, wawili hao walikwenda katika mji wa Faya-Largeau ambako kuna askari wa Ufaransa. Historia ya kuweko Ufaransa barani Afrika ambapo daima kuliandamana na utumiaji mabavu wa kikoloni inarejea nyuma karne nyingi. Filihali pia Ufaransa ikitumia nara kama za misaada, kurejesha usalama na kupambana na ugaidi imeendelea kuweko katika mataifa mbalimbali ya bara hilo.

Mazungumzo y Rais wa Chad na Jean Castex Waziri Mkuu wa Ufaransa

 

Kwa sasa Ufaransa ina vituo vya kudumu vya kijeshi katika nchi za Ivory Coast, Chad, Djibouti na Mali. Fauka ya hayo, Ufaransa ina uingiliaji wa kijeshi wa moja kwa moja katika nchi za eneo la Sahel Afrika za Mali, Mauritania, Niger, Chad na Burkina Faso, kiasi kwamba, mataifa hayo yanahesabiwa kuwa waitifaki wakuu wa nchi hiyo magharibi wa Afrika.

Hata hivyo viongozi wa Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni wameonyesha kujuta kwa uwepo wa kikoloni wa nchi yao katika bara la Afrika na kusema bayana kwamba, hatua hiyo ilikuwa ni kosa. Kama alivyokiri Rais Emmanuel Macron aliposema kwamba, kufanya ukoloni lilikuwa kosa kubwa la kihistoria la Ufaransa. Hata hivyo lililo wazi ni kwamba, walichofanya hivi sasa viongozi wa Ufaransa katika zama hizi ni kubadilisha tu mbinu zaidi na kimsingi hawajaondoka barani Afrika.

Ukweli wa mambo ni kuwa, bara la Afrika lina nafasi muhimu kwa Ufaransa, kwani taifa hilo la Ulaya si tu kwamba, linanufaika na maliasili, utajiri na hali ya kijiografia ya mataifa hayo bali kwa mtazamo wa kijeshi na kiusalama mataifa mbalimbali ya Afrika hususan ya magharibi na Sahel Afrika yana nafasi muhimu mno kwa utawala wa Paris.

Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa nchini Mali

 

Bidhaa nyingi za Ufaransa zinauzwa katika mataifa hayo na nchi hizo zinahesabiwa kuwa ni washirika wakubwa wa kibiashara wa Paris. Katika upande mwingine, maliasili na vyanzo vya utajiri vya baadhi ya mataifa hayo kama madini ya almasi na urani ya Afrika ya Kati, maliasili na vyanzo vya nishati daima vimekuwa katika mikono ya mashirika ya Kifaransa.

Abdul-Razaq Mqri, Mkuu wa Harakati ya Salam ya Algeria anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Ufaransa imewafanya mataifa ya Afrika kuwa masikini ikiwa na lengo la kufikia maslahi yake na kujenga uchumi wake. Kimsingi hatua za Ufaransa baada ya kupata uhuru mataifa ya Afrika zinahesabiwa kuwa mbaya zaidi ya zile zilizofanywa na taifa hilo wakati wa kutaka kuyadhibiti mataifa hayo.

Moja ya visingizio muhimu vya Ufaransa vya kuendelea kuwepo kijeshi barani Afrika hususan katika nchi za eneo la Sahel Afrika ambapo baadhi yazo ni makoloni ya zamani ya dola hilo la Ulaya ni kupambana na makundi ya kigaidi. Takwimu zilizotolewa zinaonyesha kuwa, Ufaransa ina askari zaidi ya 4,500 katika eneo la Sahel Afrika na ingali inaendelea kuimarisha uwepo na ushawishi wake katika nchi hizo.

 

Hii ni katika hali ambayo, askari hao wa Ufaransa hawajawa na mafanikio yoyote yale katika kupambana na ugaidi katika eneo hilo hususan nchini Mali ambako ndiko makao makuu ya vikosi vya dola hilo la bara Ulaya. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, inachokifuatilia Ufaransa si kingine bali ni kulinda maslahi yake ya kiuchumi na kibiashara katika eneo hilo.

Hivi sasa pia, safari ya Jean Castex, Waziri Mkuu wa Ufaransa huko nchini Chad ni sisitizo juu ya umuhimu wa Afrika na vituo vya kijeshi vya nchi hiyo katika bara hilo, huku ikihesabiwa kuwa ni juhudi za Paris za kulinda satwa na ushawishi wake  mbele ya washindani wake.