Waasi 44 wauawa na jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati
Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati limetangaza habari ya kuua waasi 44 waliokuwa na nia ya kuzingira na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui sambamba na kuipindua serikali ya Rais Faustin Archange Toudera wa nchi hiyo.
Katika taarifa iliyochapishwa jana Jumatatu katika mtandao wa kijamii wa Facebook, serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imesema wanajeshi wa nchi hiyo wakishirikiana na askari 'waitifaki' wamefanikiwa kuwaangamiza wapiganaji 44 katika kijiji cha Boyali, umbali wa kilomita 90 kutoka mji mkuu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mbali na wapiganaji kadhaa wa kabila la Fulani, waasi wengine waliouawa katika operesheni hiyo ni mamluki kutoka nchi za Chad na Sudan.
Msemaji wa serikali, Ange-Maxime Kazagui ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wakishirikiana na wanajeshi wa Rwanda na Russia wanafanya operesheni za kuwafurusha waasi hao, na tayari wamefanikiwa kukidhibiti kijiji cha Boda, yapata kilomita 124 kutoka Bangui.
Waasi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari waliuteka mji wa Bangassou, mashariki mwa mji mkuu Bangui, siku moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika Disemba 27 mwaka jana. Hata hivyo siku chache baadaye, askari wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA walifanikiwa kuudhibiti tena mji huo wenye utajiri wa madini ya almasi, ulioko umbali wa kilomita 750 kutoka jiji kuu la Bangui.
Januari 18, Mahakama ya Katiba wa CAR iliidhinisha ushindi wa Faustin Archange Toudera katika uchaguzi wa rais wa Disemba 27. Touadera alishinda muhula wa pili kwa kuzoa asilimia 53.1 ya kura, na kumbwaga Waziri Mkuu wa zamani, Anicet Georges aliyeambulia asilimia 21.6.