Mkuu wa zamani wa polisi Afrika Kusini asailiwa
Tume ya uchunguzi wa mauaji ya mwaka 2012 katika kijiji cha Marikana nchini Afrika Kusini imemsaili mkuu wa zamani wa polisi wa nchi hiyo.
Mtandao wa habari la Africa Time umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, tume hiyo ya uchunguzi imemsaili Riah Phiyega, mkuu wa zamani wa polisi wa Afrika Kusini kuhusiana na mauaji hayo ya mwezi Agosti 2012 katika kijiji cha Marikana cha kaskazini mashariki mwa Afrika Kusini.
Mwezi Agosti 2012, polisi wa Afrika Kusini waliwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wanaomba kuongezwa mishashara yao katika kijiji hicho na kuua waandamanaji 34.
Riah Phiyega anatuhumiwa kubariki na kuyaunga mkono mauaji ya wachimba migodi hao.
Kwa upande wake Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alilazimika kumsimamisha kazi mkuu huyo wa polisi kufuatia kuongezeka mashinikizo ya watu waliouawa kwenye maandamano hayo tangu miezi sita iliyopita.
Hata hivyo familia za wahanga hao wanataka Riah Phiyega pamoja na Nathi Mthethwa, waziri wa wakati huo wa usalama wafuatiliwe kisheria kuhusiana na mauaji hayo.